Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefika katika Kituo cha Afya Nyamsenda kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa na kutoa somo la uwajibikaji kwa Viongozi na Wataalamu baada ya kubaini kuwa wamekua wazembe katika kuchukua maamuzi.

Akikagua ujenzi wa majengo ya Mama na Mtoto, upasuaji, nk Mkuu wa Mkoa amejikuta akiingia kwenye fatiki ya kuondosha mifuko ya saruji katika makazi ya mtumishi anayeishi kwenye chumba kimoja kutokana na chumba kingine kujazwa saruji zilizoganda ambazo hazifai tena kwa matumizi.

Mkuu wa Mkoa amefafanua kuwa mnamo juni 03, 2021 serikali ilileta Tshs. Milioni 250 katika kituo hicho cha Afya kwa ajili ya ujenzi lakini pamoja na kukamilika kwa ujenzi kulitokea uzembe uliosababisha mifuko kadhaa ya saruji kaganda na kwamba waliosababisha walishachukuliwa hatua za kinidhamu.

Aidha, Halmashauri hiyo iliendelea kubaki na mifuko hiyo na kuamua kuihifadhi kwenye nyumba ya mtumishi na kusababisha adha ya kuharibu faragha kwenye kaya hiyo yenye watoto wawili ambao walilazimika kulala na wazazi wao.

Halikadhalika Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kufanya tathmini na kukarabati nyumba hiyo ndani ya siku saba ili kumpatia mazingira safi na salama ya kuishi mtumishi huyo pamoja na familia yake.

Juma Lugendo, Msaidizi wa Afya katika kituo hicho ambaye ni mtumishi anayeishi kwenye chumba kimoja katika nyumba yenye vyumba 2 kutokana na kimoja kugeuzwa kuwa stoo ya kuhifadhia saruji iliyoganda amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maamuzi ya kuondoa saruji hiyo.

Aidha, ameonesha furaha yake na kubainisha kuwa kwa sasa ataishi na familia yake kwa furaha kwani hawatakua na woga wa kuingiliwa na wadudu lakini pia kwa kuondokana na athari za kiafya ambazo wangeweza kuzipata yeye na familia yake.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.