RC MTANDA ATOA SOMO UMUHIMU WA SADAKA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameikumbusha jamii umuhimu wa kutoa sadaka kwa moyo mkunjufu kwani kwa kufanya hivyo ndio maombi na sala zinaweza kupokelewa na kujibiwa kwa haraka zaidi na Mwenyezi Mungu.
Ameyasema hayo leo machi 30, 2025 alipokuwa akizungumza katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Katoliki la Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Daima- Kome, Wilaya ya Sengerema Jimbo la Geita. Harambee iloyofanyika katika ukumbi wa Gold Crest Hotel, Jijini Mwanza.
"Katika changizo hili naomba tutoe kwa imani tukiamini kwamba Mungu atatusaidia kwa mambo mbalimbali kama magonjwa, migogoro ya ndoa hivyo toa kwa imani kuwa natoa sadaka hii ila Mungu maliza mgogoro wangu wa ndoa, Hivyo toa huku ukiomba”. Mhe. Mtanda
Aidha Mkuu wa Mkoa ameendelea kwa kusema unapotoa sadaka yakupasa kutoa kwa imani na sio kwa manung'uniko, amesema usitoe kwa sifa wala manung'uniko ni mambo ambayo Mungu ameyakataza.
“Na kama umegombana na ndugu yako kabla ya kutoa sadaka yako kapatane nae kwanza ili ubarikiwe. Ukitoa unapata heri na unaweka hazina yako mbinguni." - Mkuu wa Mkoa.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa pia ameitaka jamii kutoa sadaka kutokana na uwezo yaani isizidi wala isipungue kiwango ambacho mtu anakipata aidha amesema na ndio maana kuna sadaka inaitwa zaka ambayo huitajika 10% tu ya mapato na haitakiwi kupungua wala kuongezeka.
Naye Mhashamu Baba Askofu Flaviana Kassala Askofu wa Jimbo Katoliki Geita amesema harambee hiyo ya ujenzi wa kanisa Katoliki inatokana na umuhimu wa kanisa hilo na historia iliyopo ambapo mpaka sasa kanisa hilo limefikisha miaka 125, hivyo ujenzi huo unahusisha kulinda historia ya Kanisa na kisiwa cha kome.
“Ujenzi wa kanisa hili si kwa ajili ya Kanisa tu bali imebeba historia yetu kama Taifa, ambapo hapo awali miaka ya 1900 ilisaidia kuimarisha mahusiano kati yetu na wageni waliotoka nchi za ulaya kuleta injili”.
Aidha Mhashamu Baba Askofu ameendelea kwa kusema kisiwa cha kome kina vivutio na matarajio mengi hivyo kusherehekea miaka hiyo 125 ni kulinda pia tunu na historia ambayo kisiwa hicho kinabeba.
Awali Harambee hiyo ilikusudia kupatikana kwa shilingi milioni 500, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amechangia kiasi cha shilingi milioni 5, huku jumla kuu ya fedha taslimu na ahadi ni shilingi milioni 177. Aidha sherehe ya miaka 125 ya Kanisa hilo inatarajiwa kufanyika Agosti 17 mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.