Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wakuu wa taasisi na mashirika nchini kutenga fedha za michezo na kuzitumia kwa mujibu wa vifungu vya michezo ili kuimarisha afya ya watumishi.
Ametoa maagizo hayo leo tarehe 02 Septemba, 2025 wakati akifungua mafunzo na semina kwa Viongozi, makocha na madaktari wa Michezo kutoka shirikisho la michezo ya Mashirika ya umma, taasisi na makampuni binafsi Tanzania ( SHIMMUTA).
Amesema sera za nchi zinawataka wakuu wa taasisi na mashirika kutenga fedha na kutoa kwa wakati kwa washiriki wa michezo kwenda kujumuika na wengine wakati wa kalenda ya michezo katika mikoa mbalimbali wanayokutana.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wanaoshiriki michezo wanakua na afya thabiti hawaugui ovyo na wataleta tija kwenye ofisi kwa kupata watumishi wenye afya njema wakati wote.
Vilevile, ametoa wito kwa taasisi hizo kudhamini na kuandaa mabonanza na michuano mbalimbali ya ndani ili watumishi washiriki michezo kabla ya wakati wa kukutana kwa ajili ya michezo ya SHIMMUTA.
“Mafunzo ni sehemu ya kuboresha michezo nchini, nimeambiwa hapa wapo hadi madaktari na kweli watu wote hawa wanatakiwa kupata mafunzo ya uongozi na sio tu kutoa tiba hivyo nawapongeza maana mnawapa uwezo wa kuandaa timu kikamilifu.” Amesema Mhe. Mtanda.
Akitoa risala ya wanachama, Mwenyekiti wa SHIMMUTA Ndugu Roseline Masamu amesema mafunzo kama hayo mwaka 2023 walikua 110, 2024 walikua washiriki 114 lakini mwaka 2025 wana washiriki 130, ongezeko linaloonesha kuwa wakuu wa taasisi wanatambua umuhimu wa michezo nchini.
Aidha, amebainisha kuwa semina hiyo iliyozikutanisha taasisi 59 inakwenda sambamba na maandalizi ya michezo inayoratibiwa na umoja huo ambayo inatarajia kurindima mwezi novemba ndani ya Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.