RC MTANDA ATOA WITO KWA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi nchini katika uchaguzi mkuu 2025 kwani Serikali imejipambanua kwenye kukuza usawa, haki na uwezeshaji kwa jamii.
Mhe.Mtanda ametoa wito huo mapema leo Machi 06, 2025 kwenye uwanja wa mpira wa Nyamagana wakati akihutubia wanawake na wananchi walioshiriki maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wanawake ngazi ya Mkoa.
Mtanda amesema wanakwake ni jeshi kubwa nchini hivyo likitumika vizuri litaleta maendeleo na Serikali inaendelea kutoa usawa wa kijinsia kwenye uongozi na ndiyo maana hata Mwanza wapo viongozi wengi wa kike na 43% ya viongozi ni wanawake nchini.
"Tunazo bilioni 2.4 kwa ajili ya mikopo kwa walemavu tena kwa jinsia zote na kundi hili siyo lazima waombe mkopo kwa vikundi hata mmoja mmoja na jumla ya wataalamu wa afya 3201 wameajiriwa kuanzia 2021 hadi 2025 na kufanya huduma za afya kuimarika zaidi mkoani Mwanza." Mhe. Mtanda.
Akisoma risala ya wanawake wa Mkoa huo Mwalimu Sophia Turuya amesema wanawake nchini ni wengi zaidi ya wanaume kwa uwiano wa zaidi ya milioni moja hivyo kundi hilo likipewa fursa litakua ni chachu ya maendeleo.
Aidha, ameipongeza Serikali kwenye uboreshaji wa huduma za afya na akawasilisha ombi la kuongezwa kwa wataalamu wa afya na mazingira pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kupata nishati safi ya kupikia pamoja na mabweni ya wasichana ili watoto wa kike wasome katika mazingira salama.
Vilevile, ameutaja mfuko wa maendeleo ya wanawake kupitia vikundi vya ujasiriamali kama mkombozi wa mikopo kwa masharti nafuu kwa wanawake ambao unawapatia mitaji kupitia mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri.
Katika kunogesha maadhimisho hayo yenye kauli mbiu 'wanawake na wasichana 2025, tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji' michezo mbalimbali imerindima kama kuvuta kamba, mbio kwenye magunia, kufukuza kuku na washindi wamejipatia zawadi nono.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.