RC MTANDA AUPOKEA MSAFARA WA BALOZI KUTOKA BURUNDI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Julai 13, 2024 ameupokea Ofisini kwake msafara wa Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Balozi Gelasius Byakanwa pamoja na wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu kutoka mjini Bujumbura nchini Burundi.
Ugeni huo umewasili Mkoani Mwanza kwa lengo la kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akizungumza mara baada ya kuwapokea wageni hao Mhe. Matanda amesema Serikali ya Tanzania chini ya Mhe. Rais Samia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Burundi chini ya Mhe. Rais Ndayishimiye.
Aidha, Mtanda amewataka vijana hao kuhakikisha wanalinda amani waliyonayo kwani madhara na athari za uharibifu wa amani hiyo tayari wanazijua, hivyo amewataka kuiendeleza amani waliyonayo kwa kutokukubali kutumika kuvunja amani yao.
"Ukishashiba amani unaanza kuwaza kuharibu amani, ni lazima tujenge utaratibu wa kuthamini amani, nchi kama Burundi mna uzoefu mkubwa wa amani ni nini". Mhe. Mtanda.
Ukiwa katika nchi yako huwezi kuona thamani ya nchi uliyonayo ila ukiwa ugenini ambapo ni uhamishoni ndio utakapoona thamani ya nchi yako, Warundi lazima mjivunie Urundi wenu kwa sababu ndio thamani yenu. Ameongeza Mhe. Mtanda.
Kadhalika, Mhe. Mtanda amewasihi Wanafunzi na walimu hao kuhakikisha wanendelea kudumisha umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuidumisha na kuiendeleza lugha ya kiswahili ili pia kiweze kukidhi vigezo vya kutumika katika nyanja nzima ya teknolojia.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Burundi , Mhe. Balozi Gelasius Byakanwa amesema wao kama ubalozi waliamua kwa juhudi zote kuikuza na kuisambaza lugha ya kiswahili na wakaona waje na utaratibu wa kushindanisha wanafunzi wa vyuo vikuu katika uandishi wa insha mjini Bunjura, lengo likiwa ni kuhakikisha wanakikuza na kukiendeleza lugha adhimu ya kiswahili.
Aidha Mhe. Balozi Byakanwa amesema wako Mkoani Mwanza kujionea yale mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati kama vile mradi wa daraja la kigongo - Busisi, ujenzi wa Neli kubwa ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu.
"Nina imani hawa vijana watakua mabalozi wazuri wa lugha ya kiswahili na yale tuliyoyashuhudia hapa Mwanza na hawa wataleta watu wengi zaidi, lakini pia hawa tunaweza kuwaita wavuvi ambao watakwenda kuvua wengi zaidi waje kutalii Mkoani Mwanza".
Vijana hawa jana wameshuhudia kwa macho yao namna daraja lilivyojengwa juu ya maji, ujenzi wa Meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu na wengine pia walikua hawajawahi kupanda hata meli hivyo wamepanda hapa Mwanza, nikuhakikishie RC, hawa watakwenda kuutangaza vyema Mkoa huu wa Mwanza. Ameongeza Mhe. Balozi Byakanwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.