Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka vijana na makundi mengine mkoani humo kuchangamkia fursa za kujiajiri katika kilimo, uvuvi na ufugaji ili waweze kupata mikopo isiyokua na riba kupitia benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) inayosimamiwa na serikali.

Amebainisha hayo leo Disemba 3, 2025 wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kwa Waandishi wa Habari mkoani humo ambapo ametumia wasaa huo kuwaalika wananchi kwenda kukopa na kufanya shughuli za uzalishaji.

Mhe. Mtanda amesema kwa kipindi cha mwaka 2024/25 jumla ya Tshs. Bilioni 7.5 zimekopeshwa bila riba na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa vijana 350 wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi wa kisasa wa kutumia vizimba walio katika vikundi 47 ambapo tayari Bilioni 1.3 wamerejesha kwa awamu ya kwanza.

“Jumla ya Tshs. Bilioni 7.5 zimekopeshwa bila riba na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa vijana 350 walio katika vikundi 47 mkoani Mwanza katika kipindi cha 2024/25 wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi wa kisasa wa kutumia vizimba”. Amesema Mhe. Mtanda.

Aidha, amewataka wanahabari pia kuchangamkia fursa na kuunda vikundi vyao ili waweze kupata fursa ya kukopeshwa na kurejesha bila riba na waweze kujikwamua kiuchumi kwakua kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo imekua hodari wa kuwawezesha wajasiriamali.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari meneja wa TADB kanda ya ziwa Bw. Alphonce Mokoki amesema benki yao inalengo la kuwawezesha wakulima ili waweze kutoka katika kilimo cha kujikimu na kwenda katika akilimo cha biashara pamoja na kuiwezesha nchi kuwa na chakula cha kutosha.

Ameongeza kuwa benki hiyo imekua kinara wa kuwafungulia fursa vijana na kwamba zaidi ya Tshs. Bilioni 79.14 zimekopeshwa kwa makundi ya wafugaji, wakulima na wavuvi mkoani humo na wote katika mnyororo huo wa thamani.


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.