RC MTANDA AWAKUMBUSHA WANANCHI KUWAJALI WATOTO Yatimie
Leo Machi 26, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said GB Mtanda ameandaa Iftar kwa Watoto Yatima wanaolelewa kwenye vituo vya Watoto Yatima katika Mkoa wa Mwanza ikiwa ni sehemu ya Ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mkuu wa Mkoa amesema lengo la kufanya iftar hiyo ni kutii maagizo ya Mwenyezi Mungu ambaye yeye mwenyewe amesema mtu yeyote anaewakimbilia yatima na wajane basi amefunga hesabu na Mwenyezi Mungu.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesema imekuwa mazoea kwa kutoa iftar na chakula lakini yeye amekuja na wazo la kuboresha maisha na makazi ya watoto kwa kuwa wamekuwa wakiishia kupata chakula tu lakini mazingira wanayoishi ni mabovu.
“Tumekubaliana kuwa tutafanya utafiti tuone ni vituo gani vina uhitaji wa maboresho ya makazi au uhaba wa vitu kama vile vitanda, magodoro na vifaa vingine kisha tuone tunawasaidiaje”.
Kadhalika ametumia wasaa huo kuendelea kuwataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuitunza amani na kuendelea kuliombea Taifa, Viongozi na Serikali kiujumla chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili Taifa liendelee kuwa salama.
Naye Shekhe wa Mkoa wa Mwanza Alhajj Hassan Kabeke amemshukuru Mkuu wa Mkoa kuendelea kufanya mambo makubwa na siyo kufturisha tu bali pia kwa kuwaandalia watoto hao mahitaji mbalimbali muhimu ambayo pia itawaondolea mzigo walezi na wahisani wa watoto hao kwa kipindi fulani.
“Lakini pia Mtume wetu S.W.S anasema nyumba yoyote ambayo yatima atatendewa mema viumbe wa mbinguni wataona nyota inang’aa na nina hakika kwa hadithi hii ya Mtume huko juu wanaulizana hiyo nyota ni ya wapi wanajibiwa ni Mwanza na huyo ni Said Mtanda ametambua nafasi ya Yatima”.
Umefanya vyema Mkuu wa Mkoa ninakupongeza sana. Ameongeza Shekhe Kabeke.
Wakizungumza katika nyakati tofauti tofauti Viongozoi wa Taasisi za kifedha Mwanza walioshirikiana na Mkuu wa Mkoa katika kuandaa Iftari hiyo wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa iftar hiyo ya Yatima na kuwaleta pamoja kushiriki ibada hiyo muhimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.