RC MTANDA AWAPONGEZA TTCL UBORESHAJI MIUNDOMBINU NA HUDUMA, AWATAKA WANANCHI KUJIUNGA KWA GHARAMA NAFUU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amelipongeza Shirika la Mawasiliano nchini TTCL kwa uboreshaji wa Miundombinu na huduma za mawasiliano hususani katika simu na intaneti na ametoa wito kwa wananchi kujiunga na huduma hizo ambazo ni za gharama za nafuu kulinganisha na wengine.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo leo tarehe 11 Julai, 2024 wakati alipofanya ziara kwenye shirika hilo tawi la Mwanza kwenye eneo la Utawala Nyamagana pamoja na kwenye miundombinu ya kuendeshea huduma kwenye vituo vya Ilemela pamoja na Kiseke.
Amesema maamuzi ya matumizi ya waya za Fiber (Mkongo wa Taifa) kutoka kwenye teknolojia ya Copper zilizokuwa zinatumika hapo awali ni mapinduzi ya kiteknolojia na dhima ya dhati ya uboreshaji wa huduma tena kwa gharama nafuu.
Aidha, amewasifu TTCL kwa kuamua kutumia nguzo za Shirika la Umeme nchini kwa ajili ya kusambazia waya za shirika hilo kwani itarahisisha kuwafikia wateja wengi zaidi na kwa gharama ya chini ya uendeshaji kwani tayari wateja wanaofikiwa na nishati ya umeme kwa nguzo hizo wamesambaa kote nchini.
Awali, Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Mwanza Bw. Jalili Senkopwa amebainisha kuwa juhudi za uboreshaji zilianza mwaka 2017 hususani baada ya kuchukua shughuli za lililokua shirika la Simu kwa asilimia 100.
Aidha, amesema bidhaa za simu na intanenti zimeboreshwa na kwa kushirikiana na mfuko wa mawasiliano (USCAF) wanaweka minara kwenye maeneo yaliyokosa mvuto hususani kwenye visiwa vya Maisome, Bukimwi na Bezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.