RC MTANDA AWATAKA AFD KUTOA BARUA YA KUTOKUWEPO NA KIPINGAMIZI KATIKA MIRADI INAYOENDELEA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Juni 04, 2024 ofisini kwake amekutana na kufanya kikao kifupi na Mkurugenzi wa Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la ufaransa (AFD Agence Francaise de Developpment) Bibi Hellen Ngarmin ambaye yupo Jijini Mwanza kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na MWAUWASA na iliyopangwa kutekelezwa.
Akizungumza katika kikao hicho RC Mtanda ametoa rai kwa AFD kutoa barua ya kuondoa vipingamizi katika mradi wa ujenzi ili kuruhusu kuendelea na hatua inayofuata kwenye mchakato wa ujenzi wa mradi wa usambazaji mabomba na ujenzi wa matenki katika upanuzi wa mradi wa maji Butimba.
Aidha Mhe. Mtanda amesema Serikali na Wananchi wa Mwanza wanatamani kuona huduma ya usambaji maji inatekelezwa katika maeneo husika na kukamilika kwa wakati ili jamii iondokane na adha ya upungufu wa maji hivyo ni wakati sasa wa kuongeza kasi kwenye taratibu za utekelezaji.
"Mradi wa Butimba ni muhimu sana kwa kuwa hapo kabla tulikuwa na mradi tegemezi wa chanzo cha kapripoint ambao haukuwa unatosheleza mahitaji hivyo kukamilika kwa mradi huu utawanufaisha watu wengi". Amesema RC Mtanda.
Mhe. Mtanda amesema pia Mwanza ni Mkoa wa Pili kwa ukubwa na ni mji wa kiuchumi hivyo uboreshaji wa sekta ya maji utapelekea watu wengi kuvutika na kufanya uwekezaji na makazi hali ambayo itapelekea uchumi wa Mwanza kukua na kuongeza muingiliano wa watu kutoka Afrika Mashariki ambao wameunganishwa na ziwa Viktoria.
Sambamba na ufadhili wa mradi wa maji wa Butimba RC Mtanda amewashukuru AFD kwa kuendelea kufadhili miradi mingine ya kimkakati kama vile ujenzi wa matundu 104 ya vyoo kwa shule za msingi, masoko na Zahanati katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela.
Naye Mkurugenzi wa Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la ufaransa (AFD Agence Francaise de Developpment) Bibi Hellen Ngarmin amesema anefurahishwa na kasi ya maendeleo ya usambaji wa huduma ya maji hasa kwa wakazi wanaoishi katika milima.
Viongozi hao kutoka Shirika la Maendeleo la ufaransa (AFD Agence Francaise de Developpment) Wametembelea Soko la Mwaloni pamoja na miradi ya maji taka na mradi wa upanuzi wa chanzo cha Maji Safi Butimba awamu ya pili (Phase II)
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.