RC MTANDA AWATAKA RUWASA KUFIKISHA MAJI MWASONGWE - MISUNGWI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Misungwi kuhakikisha wanafikisha Maji kwenye kijiji cha Mwasonge kupitia mpango wa upanuzi wa mradi wa Maji wa Kigongo- Busisi wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 6.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Septemba, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika ziara yake aliyoifanya mahsusi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuibuliwa kero hiyo dhidi ya RUWASA.
Mhe. Mtanda amesema RUWASA ina wajibu wa kutumia ubunifu kuhakikisha wananchi wanafikishiwa maji kwa kutumia miradi mikubwa inayotekelezwa sehemu mbalimbali kwa kutumia chanzo cha maji ya ziwa victoria na akawataka ndani ya siku 4 kuhakikisha wanatoa elimu kupitia mkutano wa kijiji kuhusu lini wanawafikishia huduma hiyo.
Naye, Kaimu Meneja wa RUWASA Misungwi Mhandisi Richard Mlilwa amebainisha kuwa mapema mwaka 2025 wananchi wa Mwasonge watafikishia Maji kupitia Mradi huo ambapo tayari usanifu umeshafanyika na kupata mtandao wa kilomita 25 na kwamba wataweka vituo 12 vya kuchotea Maji na tanki lenye ujazo wa Lita 650,000.
Aidha kufuatia kero ya ndugu Issa Omary aliyoiwasilisha katika mkutano huo inayohusiana na masuala ya usalama, Mkuu wa Mkoa ameliagiza jeshi kuhakikisha ndani ya siku 7 wanawakamata wahalifu waliovunja maduka 5 na kuiba mali kwenye kijiji hicho usiku wa kuamkia Septemba 13, 2024 na wafikishwe mahakamani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.