RC MTANDA AWATAKA SUNGUSUNGU KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka askari Jamii wa Jeshi la Jadi (Sungusungu) Mkoani humo kufanya kazi zao kwa kuzingatia misingi ya haki na sheria pasipo kumuonea mwananchi yoyote.
Mhe. Mtanda ametoa maagizo hayo leo Februari 20, 2025 kwa nyakati tofauti tofauti alipokuwa akizungumza na Sungusungu Wilayani Kwimba ambapo amesema ameamua kufanya ziara hiyo maalumu kwa lengo la kuona shughuli zinazofanywa na jeshi hilo la jadi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amelipongeza jeshi hilo kwa kuwa walinzi imara wa raia na mali zao lakini kubwa zaidi kwa kusaidia pia katika ulinzi wa mifugo ambapo kwa kiasi kikubwa wizi wa mifugo kwa maeneo ya vijijini umepungua kutokana na uimara wa Sungusungu.
Ikumbukwe pia jeshi hilo la jadi katika sherehe za kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa zilizofanyika Mkoani Mwanza Oktoba 14, 2024 jeshi hilo likinogesha zaidi sherehe hizo kwa kuhudhuria kwa wingi na gwaride la kipekee, Mhe. Mtanda ametumia wasaa huo pia kuwapongeza kwa ushiriki wao.
“Nimekuja pia kuwapongezeni na niwahakikishie Rais Dkt. Samia anawatambua na aliwaona siku ile ya kilele cha mbio za Mwenge mwaka jana pale CCM Kirumba hivyo endeleni kuchapa kazi”. Mtanda.
Mkuu wa Mkoa amesema pia lengo lingine la ziara hiyo ni kuja kujionea maendeleo ya sungusungu ambapo kwa hapo baadae amepanga kufanya tamasha kubwa ambalo litalenga kujadili na kutoa elimu ya uchaguzi, usalama kueleka kipindi cha uchaguzi pamoja na michezo na burudani.
Mkuu wa Mkoa ametembelea na kufanya mkutano na Sungusungu katika maeneo mbalimbali ya Wilaya Kwimba akiwakumbusha pia umuhimu wa kutunza amani katika maeneo yao na Taifa kwa jumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.