RC MTANDA AWATAKA VIJANA WANAVYUO KUTOHARAKIA MAISHA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Vijana kutoka Vyuo Vikuu na vya Kati Mkoani humo kuacha tamaa ya kukimbilia kutamani kupata vitu au mali ambavyo hawana uwezo navyo kwani inachochea ukatili wa kijinsia.
Mhe. Mtanda ametoa rai hiyo mapema leo tarehe 20 Novemba, 2024 wakati akizindua Kampeni ya Kampasi Salama inayotekekezwa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Halikadhalika, ametumia jukwaa hilo kuwasihi vijana kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kuwapeleka kwenye hatari ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia na amewataka kutumia wakati vema kwa ajili ya kuwa salama na kujibidiisha katika masomo.
"Mzazi kakuleta hapa kwa imani kubwa sana na wewe inakuaje ukifika chuo usijisimamie na kujitambua ili uweze kuwa kijana bora ukasoma kwa bidii na kuandaa kesho yako bora." Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Mtanda amebainisha kuwa Serikali kupitia wizara ya maendeleo ya jamii inaendelea kuratibu upatikanaji wa afua mbalimbali za utekelezaji wa sera ya kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini ikiwemo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Vilevile, amewapongeza UNESCO na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya jamii kwa kutekekeza mradi wa O3 PLUS ambao malengo yake ni kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyo vikuu na vya kati.
Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha SAUT Mwanza Prof. Hoseah Regoshora amewashukuru UNESCO kwa kuwa sehemu ya kampeni ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi kwa kuwajengea uwezo na kufadhili tafiti.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNESCO Nchini Tanzania, Bw. Michael Toto amesema wamedhamiria kutokomeza kabisa ukatili kwa wanafunzi wawapo kwenye kampasi zao na ndio maana wameamua kutoa elimu ya umuhimu wa usalama wa watoto wawapo chuoni kwa ufanisi katika masomo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.