RC MTANDA AWATAKA VIONGOZI WA USHIRIKA MWANZA KUJIEPUSHA NA UBADHIRIFU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Viongozi na Watendaji wa Vyama vya ushirika katika Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wakati wote wanasimamia na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013 na kanuni zake.
Mkuu wa Mkoa amebainisha kuwa masharti ya vyama hivyo ni pamoja na kujiepusha na vitendo viovu kama vile ubadhirifu/wizi, matumizi mabaya ya madaraka, kutokuwajibika na uzembe maana vitendo hivi vinasababisha Vyama vya Ushirika kuendelea kuzorota na kushindwa kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wanachama na wakulima kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo mapema leo Machi 21, 2025 alipokuwa akizungumza na Wanaushirika waliohudhuria mkutano mkuu wa 33 uliofanyika katika Ukumbi wa Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza.
Kadhalika Mhe. Mtanda ameitaka Tume ya Maendeleo Tanzania kuendelea kusimamia na kuhakikisha ukaguzi wa mara kwa mara unafanyika katika Vyama vya Ushirika na dosari zinazobainika zinafanyiwa kazi mara moja.
“Kwa kufanya hivyo itasaidia kuhakikisha vyama vinaendeshwa katika misingi ya haki lakini pia rasilimali za Ushirika zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa”.
Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza Bi. Hilda Boniface amesema Mkutano Mkuu huo wa ushirika umelenga kupitia na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mafanikio, hatua mbalimbali zilizofikiwa na chama hicho pamoja na kujadili mipango ya mwakani.
Aidha amesema kupitia Mkutano huo pia kutakua na mjadala wa demokrasia na wazi kwa wanachama wote wataruhusiwa kutoa maoni yao juu ya kile ambacho bodi itakileta mezani ili kupata maoni yatakayojenga ushirika Mkoani Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.