RC MTANDA AWATAKA WAFANYABIASHARA WANAOFANYA MNADA BARABARANI KURUDI KWENYE SOKO RASMI LA KILOLELI
Mhe. Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewataka wafanyabiashara wilayani Ilemela kufuata sheria za nchi kwa kufanya shughuli zao kwenye masoko rasmi na Halmashauri isimamie hilo kwa kupunguza Minada ya barabarani na kuhamasisha wabaki kwenye masoko yaliyopangwa.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 05 juni, 2024 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Kiloleli lililopo kwenye kata ya Ibungilo wilayani Ilemela baada ya kubaini wafanyabiashara wadogo kususia Soko hilo lenye miundombinu rafiki na kujikita kwenye magulio ya mnada yanayofanyika kwenye hifadhi za barabara.
"Kukaa kwenye masoko kuna faida kubwa ya kwanza ikiwa ni kutambulika nani yupo wapi na anafanya biashara gani, watu wafuate sheria wakae kwenye masoko sio kuendekeza minada inayofanyika barabarani, tupunguze magulio ili mabenki wajue wanawapata wapi kuwakopesha na hata Mikopo ya Rais Samia ikishakua tayari itakua rahisi kuwapata." Amesisitiza Mhe. Mtanda.
Akibainisha Miradi mikubwa inayotekelezwa Mwanza, Mtanda amesema Soko Kuu la Mjini Kati linalojengwa kwa zaidi ya shilingi Bilioni 20 linaelekea kukamilika na kwa sasa limefikia 95% ya ujenzi na Serikali inatarajia kuongeza Bilioni 3 ndani ya mwezi huu ili likamilike na waganyabiashara zaidi ya elfu mbili watarudi kuendelea na biashara kwenye soko lile la kisasa.
"Nimetoa wito kwa maeneo yote niliyopita kwamba Askari wa Jeshi la akiba kazi yao sio kupiga wananchi na kunyang'anya biashara nasi tutawafikisha mahakamani wanaofanya hivyo bali wanapaswa kukamata na kuwafikisha kwenye vyombo husika." Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala amesema wapo tayari kutekeleza maagizo hayo na kwamba wamejipanga kuboresha miundombinu kwenye masoko yao na kwa mwaka wa fedha unaoendelea wametumia zaidi ya Milioni 180 kukarabati miundombinu kwenye masoko lakini bado machinga wamejikita kufanya biashara kwenye hifadhi za barabara kwa kigezo cha mnada.
Magabe Ligata, mwenyekiti wa Soko la Kiloleli na mwenyekiti wa Wafanyabiashara na Masoko wilayani Ilemela ametoa kwa wafanyabiashara wenzake kurudi kwenye soko hilo ili maeneo ya nafaka, ndizi, matunda na nguo yapate wafanyabiashata kuliko hali ya sasa ya kuwa na wafanyabiashata 386 pekee kwenye soko hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.