RC MTANDA AWATAKA WALIOVISHWA NISHANI WAKAWE MABALOZI WAZURI KWA WENGINE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewapongeza maafisa, wakaguzi na askari wa Jeshi la Zimamoto waliovishwa nishani na kusema mafanikio yao yatakua chachu kwa wengine kufikia na hata kuzidi viwango vya ubora wa kufanya kazi.
Akizungumza leo katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Mkoani humo Bw. Balandya Elikana amebainisha heshima hiyo waliyopewa na Rais Samia wana wajibu wa kuja na matokeo chanya ya kufanya kazi kwa weledi na nidhamu.
"Nishani zilizotolewa leo ni kumbukumbu kwa sisi tuliopo na wanaokuja kwamba hawa ni miongoni mwa waliofanya vizuri hivyo niwatake mkawe mabalozi wazuri kwa wengine".Balandya
Aidha amelipongeza Jeshi hilo la Zimamoto na Uokoaji kwa kazi nzuri na ya mfano kwa wengine, amesema limekuwa likifanya kazi kubwa na nzuri ya kuokoa maisha na mali za watu.
"Hongereni sana. ninatambua na kufarijika na jitihada zinazoendelea kufanyika na mafanikio ya kutia moyo kupitia marafiki wa zimamoto". Mtendaji wa Mkoa
Mara baada ya kuwavisha nishani maafisa, wakaguzi na askari 25 wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na jirani Kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga amewataka kudumisha nidhamu kazini.
Aidha Kamishna Jenerali Masunga amewataka wale ambao hawakupata nishani hizo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa kwani zoezi hilo halijaishia leo bali kuna nishani nyingi zitaendelea kutolewa.
"Tukachape kazi kwa bidii, tuwe na tabia njema, tuendeleze nidhamu katika vituo vyetu vya kazi, hiyo ndio njia pekee itakayohusika katika kuwafanya mkatunukiwe nishani". Kamishna Jenerali Masunga..
Wakati huo huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana mapema leo asubuhi Ofisini kwake amefanya mazungumzo na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.