RC MTANDA AWATAKA WANA MWANZA KUENDELEA KUDUMISHA AMANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kuilinda na kuitunza amani tuliyonayo kwani imejengwa kwa muda murefu na kutokukubali kuruhusu watu wachache ambao hawaitakii mema nchi yetu kuja kuivuruga amani hiyo.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na Waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria katika sherehe za Maulid zilizofanyika katika Msikiti wa Raudhwa, Lumumba, Jijini Mwanza ambapo Maulid hiyo imeongozwa na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally.
Mhe. Mtanda amesema Taifa haliwezi kujadili maendeleo kama hakuna misingi imara ya amani, hatuwezi kusonga mbele kama ndani hatuna amani, hivyo ni muhimu sana kuilinda na kuitetea amani hiyo ili tuweze kuwa na uwanda mpana wa kujadili na kuwaletea wananchi maendeleo.
"Mhe. Mufti ulitoa wito kwenye Baraza la Maulid kule Geita kukemea vitendo vya ukatili na uvunjifu wa amani, mimi nikuhakikishie Serikali ya Rais Samia na mimi nikiwa Mkuu wa Mkoa sitakubali kuona amani ya Wana Mwanza na Watanzania inavunjwa" Amesema Mhe. Mtanda.
Aidha amesema yeye kama Mwenyekiti wa kamati ya Usalama Mkoa watafanya kazi usiku na mchana ili kuwalinda WanaMwanza na Wananchi wote wanaoingia na kutoka Mkoani humo.
Sambamba na hayo RC Mtanda ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapokutana na changamoto au tatizo lolote kwa kupiga simu kwa serikali na wao watakuja na kutoa msaada.
"Hata ukipiga simu saa nane za usiku sisi tutakuja" Ameongeza RC Mtanda.
Naye Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally amesema amani sio kitu cha kuchezea tuendelee kuilinda amani yetu na kutokukubali kufanya jambo lolote bila ya kufikiri kwanza kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kupelekea majuto.
"Uislamu ni dini ya kufikiri na kufikiria kabla ya kufanya maamuzi kwa kila jambo hilo ndilo linalotakiwa na huo ndio uislamu thabiti".
Aidha Mhe. Mufti amewataka Waislamu hao kuungana na kumsaidia Mkuu wa Mkoa na yeye binafsi amesema anamjua sana ni mtu mzuri, ni mtu safi anaependa kuwatumikia wananchi wa dini zote japo yeye ni muislamu hivyo wamuunge mkono.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.