RC MTANDA AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI, AWATAKA WATUMISHI KUWAJIBIKA KUTUMIKIA WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka watumishi Mkoani humo kufanya kazi kwa kujituma katika kuwatumikia wananchi na kutimiza wajibu bila kusubiri kuagizwa ili kuleta tija kwa Taifa.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo tarehe 12 Machi, 2025 wakati akihutubia baraza la wafanyakazi la watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Rock City Mall, Ilemela.
Amesema, mtu akifanya kazi kwa kujituma atapata mshahara kihalali na kwa Mwenyezi Mungu atapata thawabu kutokana na ibada aliyoifanya kupitia kuwajibika bila kuchoka.
"Watu wengi wanadai haki lakini hawatimizi wajibu, hiyo sio sawa kwanza ni dhuluma ni lazima kila mmoja abadilike na kuchapa kazi ndipo afurahie mshahara anaoupokea kutoka Serikalini." Amesisitiza Mhe. Mtanda.
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ni lazima wawe na mwenendo wa maadili wakati wote kuanzia mavazi hadi lugha wanazozitoa kwa wananchi ni lazima ziwe na staha pamoja na kuacha tabia za kukopa pesa ovyo. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Halikadalika, amebainisha kuwa katika bajeti ya mwaka 2024/25 Ofisi yake imetumia Milioni 171.6 kulipa madeni kwa watumishi 53 na kupandisha vyeo kwa watumishi 102 na amewahakikishia watumishi kuwa Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi.
Naye Mwenyekiti wa baraza hilo Bwana Balandya Elikana amesema baraza hilo lina manufaa makubwa ikiwemo kushirikisha wafanyakazi kutoa maoni na kupokea changamoto za watumishi na kuzifanyia kazi kupitia vikao mbalimbali vya kisheria hususan kwenye idara.
Awali, wajumbe wa baraza hilo walifanya uchaguzi ambapo bwana Gapchojiga Fabian ameshinda nafasi ya Katibu na Bi. Susan Ndunguru Katibu Msaidizi wa baraza hilo na mara moja viongozi hao wameanza miaka mitatu ya kutumikia nafasi zao kwa awamu ya pili mfululizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.