RC MTANDA AZINDUA BODI YA PAROLE YA MKOA
Leo Septemba 12, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezindua bodi ya parole ya Mkoa huo kupitia kikao kilichofanyika kwenye gereza la Mkoa la Butimba lililopo Kata ya Butimba Wilayani Nyamagana.
Akiongea na wajumbe wa bodi hiyo Mhe. Mtanda amewataka kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya bodi ya Parole nchini ili kutenda haki katika maamuzi ya kupendekeza kwa wafungwa wanaopaswa kupewa msamaha na kupunguziwa adhabu
Amesema, utaratibu wa msamaha kwa wafungwa unaotolewa na Mhe. Rais una vigezo vyake na zinapaswa kufuatwa ikiwemo taarifa ya magereza dhidi ya wafungwa husika na siyo kuwaachia kwakua kuna msongamano gerezani.
Aidha, ameipongeza bodi hiyo kwa kuwa na wajumbe kutoka maeneo kadhaa ya kisheria kama jeshi la polisi na ofisi ya mashtaka huku akibainisha kuwa itasaidia kupata vielelezo vinavyohitajika kwa wakati pindi vinapohitajika kwa ajili ya msamaha.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Masudi Juma Kimolo amesema kuaminiwa kwa wajumbe hao na waziri wa Mambo ya Ndani kuendane na kuwajibika na kuisaidia Serikali kubaini wafungwa wenye sifa ya kuachiwa kutokana na kukidhi sifa na si vinginevyo.
Aidha, ameitaka bodi hiyo iliyoteuliwa rasmi Januari 1, 2024 ilenge kusaidia juhudi za Serikali kupunguza msongamano magerezani, kurekebisha sera kutunza nidhamu na kurekebisha wahalifu kwenye magereza yote Mkoani Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.