RC MTANDA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA ARDHI KWA AJILI YA KUJENGA MAKAZI YA WAZEE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Halmashauri Mkoani humo kutenga maeneo maalum katika mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuhakikisha wanajenga makazi ya kulea wazee ili kuwahakikishia huduma bora.
Mhe. Mtanda ametoa rai hiyo wakati akizungumza na jumuiya ya wazee wa wilaya ya Sengerema katika mkutano wake alioufanya leo Juni 10, 2024 alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na makundi mbalimbali wilayani humo.
"Sisi ni wazee watarajiwa, mipango yote tutakayoweka itatusaidia wenyewe siku za usoni hivyo ni lazima sasa tutenge maeneo ya kujenga makazi ya malezi na mwakani tuanze ujenzi ili wazee wakae sehemu moja na tupeleke huduma za kijamii." Mkuu wa Mkoa.
Aidha, amesema katika kuhakikisha wazee wanakua na malezi bora ni lazima familia iwajibike kuwatunza na watoto wawalee wazee maana wao tayari wamelelewa na kusomeshwa vizuri hadi kufika hapo walipo hivyo ni lazima wathamini upendo huo ambao pia unasisitizwa na maandiko ya dini.
Vilevile, ametoa wito kwa watumishi wa afya kuhakikisha wanatoa huduma za afya kwa wazee bila malipo kwa mujibu wa sera zetu na amezitaka familia kuhakikisha malezi ya mtoto yanaanza kwenye unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa zaidi ya miaka miwili na nusu ili kuwahakikisha afya njema.
Halikadhalika, amewataka wazee kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kumuombea awe na afya na siha njema kwani anaonesha kwa vitendo upendo wake kwa kundi hilo kwa kuwaboreshea huduma za afya ikiwepo uwepo wa madirisha ya wazee ya kuwahudumia kwa kipaumbele.
Mhe. Hamis Tabasam, Mbunge wa Sengerema amesema kuwa Jumuiya ya Wazee wilayani humo ina jumla ya wajumbe 640 na kwamba adha kubwa wanayoipata kwenye huduma za jamii ni gharama kubwa za matibabu hivyo wanaomba kupatiwa bima za afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.