RC MTANDA AZITAKA NCHI WANACHAMA KUENDELEA KUDHIBITI UHALIFU UKANDA WA ZIWA VICTORIA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa nchi wanachama kuendelea na uthibiti na jitihada za kuondoa vitisho na uhalifu kuzunguka ziwa Victoria ili kuwaletea wananchi maendeleo kupitia shughuli za kiuchumi za uvuvi wanazofanya.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo mapema leo Jumanne 21 Mei, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha tatu cha kuimarisha usalama wa raia wanaofanya kazi katika ziwa Victoria kutoka Kenya, Uganda na Tanzania kilichoandaliwa na Shirika la Kimataifa linalihusika na masuala ya Uhamiaji (IOM).
"Wananchi wa Kenya, Uganda na Tanzania wanajivunia na uwepo wa ziwa Victoria lenye maji safi duniani na ni kitovu cha biashara na maisha kwa ujumla hivyo ni lazima tuhakikishe tunaandaa mipango ya kuhakikisha tunaondoa vitisho vyote vya kiusalama chini ya wadau wetu Serikali ya Marekani kwa kupitia mradi wa IOM", Mhe. Mtanda.
Amesema, ni wajibu wa Serikali za nchi zote tatu kuwa na mipango ya muda mfupi na mirefu ya kuhakikisha matukio mbalimbali yanayotishia amani kwa kuwa na uhalifu mipakani yanazuiliwa na kwamba kamisheni mbalimbali zinazofanya kazi kwenye bonde la ziwa hilo zinatakiwa kuwa msaada pia kwenye suala hilo nyeti.
Aidha, ametoa wito kwa wizara zinazohika na masuala ya usalama na undelezaji maliasili maji kutoka kwenye nchi wanachama kuweka mipango ya muda mrefu kupitia bajeti za nchi wanachama kuhakikisha utapoisha mradi wa IOM kunakua na muendelezo wa juhudi za uthibiti wa uhalifu kwenye mipaka ya ziwa Victoria.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti anayemaliza muda wake Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji kutoka Uganda Marcellino Kyamutetera amesema kwa kipindi chote akiwa kwenye uongozi amehakikisha nchi wanachama zinaongeza mahusiano ya kikanda katika kuhakikisha wanazuia kwa pamoja uhalifu wa mipakani.
Ndugu David Hofmeijer kutoka IOM Ofisi ya Tanzania amesema kikao kazi hicho kinalenga kuimarisha uhusiano na kukumbushana namna bora ya kuendelea kuboresha ulinzi kwenye mipaka ya nchi wanachana yanayolenga kukabiliana na uhalifu wa Kimataifa na tishio kwenye mipaka ya nchi wanachama.
Akitoa neno la ukaribisho, Kamishna Msaidizi kutoka Sekretarieti ya kupambana na usafirishaji wa binadamu (ATS) Ahmad Mwen-dadi ametumia wasaa huo kuwashukuru IOM na nchi wanachama kwa kuendelea kulinda mipaka ya nchi na kufanikisha malengo ya mradi huo.
Ameendelea kwa kusema bandari za nchi wanachama zote zipo salama ikiwa ni kutokana na ushirikiano mkubwa uliofanywa kwa pamoja kutoka 2023 ambao IOM imekua ikitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa kutoka majeshi ya Uhamiaji, Polisi na wanamaji na kwamba mradi huo una msaada sana kwenye kuimarisha biashara na forodha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.