RC MTANDA AZUNGUMZA NA WAZEE WA KWIMBA AWAAHIDI KUMALIZA KERO ZA MAJI NA BARABARA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema Serikali ipo mbioni kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa Ngudu na wote wilayani Kwimba kwa kujenga mradi mkubwa pamoja na kuharakisha uwekaji Lami kwa kilomita 3 za mjini na baadae kupeleka hadi Mabuki.
Mhe. Mtanda ametoa ahadi hiyo leo Juni 06, 2024 wakati akizungumza na Wazee wa Kwimba katika kikao chake kifupi alichoketi nao kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
"Leo nimefanya kazi kama ya Tomaso maana nimeona na kuamini kuwa Ngudu na Kwimba kwa ujumla wanapata adha ya barabara na nawaahidi tutaanza kujenga hizo Kilomita 3 za hapa na baadae tutatafuta fedha ili kuunganisha Kilomita zote 26 hadi barabara kuu kule Mabuki", amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, ametoa wito kwa vituo vya afya, zahanati na Hospitali ndani ya Wilaya hiyo na zingine kuhakikisha wanatoa upendeleo kwa wazee kwa kuimarisha madirisha ya kuhudumia wazee wanapofika kwenye vituo hivyo kupata huduma za afya.
"Watoto wa kike wapewe fursa ya kusoma, ni uwekezaji mkubwa kuliko kupokea ng'ombe wa mahari, tuwaache wasome ili baadae wawe madaktari wazuri na waweze watusaidie" amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Naye, Mzee Edward Seneda Mwenyekiti wa Wazee Kwimba amezungumzia furaha yake kwa kupata fursa ya kuzungumza na Mkuu wa Mkoa na kueleza changamoto zao na kuzichukua kwa ajili ya kuzifanyia kazi siku za usoni.
Shekhe wa Wilaya na Kiongozi wa Kamati ya Amani na Kiongozi wa Sungusungu wametumia wasaa huo kushukuru Serikali ya wilaya kwa kuwajali na kushirikiana nao kwenye shughuli mbalimbali na wamemtakia Mkuu wa Mkoa kheri katika shughuli zao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.