RC MTANDA: MALEZI YA MABAVU CHANZO CHA KUMJENGEA HOFU MTOTO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw.Balandya Elikana amewataka Wazazi na Walezi kuzingatia wajibu wa malezi bora kwa watoto maana yana mchango mkubwa katika kuwajengea maadili mema.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo Juni 16,2024 kwenye ukumbi wa Gold Crest katika siku ya maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika,Balandya amebainisha malezi sahihi ni kujenga urafiki na ukaribu na mtoto na siyo vinginevyo.
Mtendaji huyo wa Mkoa amesema Wazazi wengi wanaamini kuwa matumizi ya nguvu na ukali (malezi ya mabavu) ndio njia sahihi ya malezi kwa watoto ambapo amesema madhara ya njia hiyo ni kumjengea hofu mtoto hivyo kuondoa dhana ya uthubutu katika ubunifu.
"Pia matumizi ya nguvu yanaweza kuudhuru mwili wa mtoto, vile vile mtoto anaweza kuathirika kisaikolojia madhara ambayo yanaweza kudumu maisha yake yote".amesisitiza Balandya
Aidha ametoa rai kwa wazazi kuachana na malezi ya kuwadekeza watoto kwa kuwapatia chochote wanachohitaji hata kama sio muhimu ambapo amesema madhara yake ni kumjengea mtoto mtazamo kuwa kila kitu kinapatikana kirahisi.
"Hisia hizo zinaweza kuendelea katika maisha yake yote, kujenga familia na taifa la kuamini katika njia za mkato na sio kupata kwa jasho - Tunashuhudia wizi na ubadhilifu ili kutimiza azma hiyo".
Akisoma risala ya watoto wa Mkoa wa Mwanza kwa mgeni rasmi, mtoto Josephine Bakita amesema wanaipongeza Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata haki za msingi hususani elimu kwani imefanikiwa kujenga shule nyingi nchini na kuweka mfumo wa elimu bila malipo kwa Shule zote, watoto wengi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu wanapata elimu sawa.
Sambamba na hayo pia amewasilisha changamoto zinazowakabili watoto amesema wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa miundombinu rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu shuleni, upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na uhaba wa Walimu wenye taaluma ya elimu jumuishi.
Akijibu baadhi ya changamoto zilizowasilishwa Balandya amesema kuwa Serikali Mkoani Mwanza kwa kushirikiana na sekta binafsi wamekuwa wakishirikiana katika upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia hivyo kama kuna mtoto yoyote mwenye uhitaji basi afike Ofisi ya Mkuu wa Mkoa aweze kupatiwa vifaa hivyo, aidha suala la uhaba wa walimu na miundombinu rafiki amesema ameyachukua kwa ajili ya utekelezaji.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2024 ni "Elimu Jumuishi kwa Watoto Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.