RC MTANDA NA BALOZI WA ITALIA TANZANIA WAKUBALIANA KUANDAA KAMBI YA MATIBABU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewasilisha ombi kwa Balozi wa Italia nchini Tanzania Mhe. Giuseppe Sean Coppola la kuanzisha kambi maalumu ya matibabu Mkoani humo, ombi ambalo limekubaliwa na Balozi huyo anbaye amesema litaratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Mhe. Mtanda ametoa ombi hilo leo Oktoba 02, 2024 wakati akizungumza mara baada ya kumpokea Balozi huyo Ofisini kwake, aliyewasili Mkoani humo kushiriki Kongamano la pili la Kudhibiti Saratani Duniani lililoandaliwa na kuratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na kufanyika katika Ukumbi wa Malaika Hoteli Wilayani Ilemela.
Mhe. Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza ni Mkoa mkubwa wenye idadi ya watu wengi baada ya Mkoa wa Dar es Salaam hivyo kuanzisha kambi hiyo itasaidia kuondoa kadhia kwa watu wenye uchumi mdogo ambao wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi mbalimbali na kushindwa kupata matibabu kutokana na kushindwa kumudu gharama za tiba.
Aidha Mhe. Mtanda pia amemtaka Balozi huyo kuleta wawekezaji ambao watasaidia katika kuanzisha viwanda vya chakula cha samaki na kusambaza vyakula hivyo kwa wafugaji wa samaki wa vizimba ambao kwa sasa wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa chakula.
"Kama utatusaidia tukapata wawekezaji wazuri katika viwanda vya chakula cha samaki nina imani utakuwa umetusaidia sana". Mhe. Mtanda.
Naye Balozi huyo wa Italia amesema kuhusu suala la huduma ya kambi ya matibabu wanaweza kuanza kwa kufanya walau mara moja kwa mwaka na baadae wakaendelea, Aidha pia amemhakikishia Mhe. Mtanda pia kuhusu suala la wawekezaji amelichukua kwa utekelezaji.
Sambamba na hayo Mhe. Balozi Coppola amesema yuko tayari kushirikiana na Serikali ya Mkoa katika masuala ya utalii, madini na kwamba kwa wakati wowote yeye na timu yake watatoa ushirikiano wa kutosha.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Nchi ya Italia imekuwa na mahusiano ya pande mbili yenye mizizi ya kina tangu kuimarishwa kwa uhusiano rasmi wa kidemokrasia mwaka 1970 ambapo Tanzania ilifungua rasmi Ubalozi wake Roma mwaka 1972 huku Ubalozi wa Italia ukifunguliwa rasmi nchini Tanzania mwaka 1961.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.