Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel ametoa agizo kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo Ngusa Samike kumuandikia barua Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG kuja Mwanza na kuchunguza mwenendo mzima wa Vikundi vyote vilivyopatiwa Mikopo ya Makundi Maalum na Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya kubainika zaidi ya Shilingi Bilioni 3 kutolewa nje ya utaratibu.
Mhe Gabriel ametoa agizo hilo baada ya kupata taarifa ya mwenendo wa utoaji wa Mikopo hiyo kutoka Kamati Maalum aliyoiunda ili kuchunguza mchakato wa utolewaji wa fedha hizo iliyobaini Vikundi 156 ndiyo Halmashauri hiyo ina taarifa zao kati ya 337 kutoka kata 10 miongoni mwa 18 zilizopo ndani ya Wilaya hiyo.
"Nimelazimika kuitisha kikao hiki baada ya kupokea ripoti ya kamati ya kuchunguza mchakato mzima wa utolewaji wa Mikopo hii,hali siyo nzuri na nimeona ni vyema tukutane,tushauriane na kuchukua hatua lengo hizi fedha zirudi katka mzunguko"
Mkuu wa Mkoa Mhe Gabriel ameagiza Watumishi wote wa Halmashauri hiyo wanaohusika kuratibu Mikopo hiyo wahakikishe waliowakopesha wamerejesha ili walengwa ambao ni Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu wanufaike na fedha hizo ambalo ni lengo la Serikali.
"Zaidi ya Shilingi Bilioni 3 kutolewa nje ya utaratibu ni nyingi sana,hizo siyo fedha za sadaka ni lazima zirudi,haiwezekani Vikundi vingine vilivyopewa Mikopo ni vya Wanawake lakini ndani yake kuna Wanaume huu ni uchotaji wa wazi wazi wa fedha za Serikali"
Amesisitiza Vikundi vyote 680 vilivyopata Mikopo hiyo Wilayani Nyamagana vifuatiliwe na taarifa zao zijulikane baada ya ripoti kuonesha ni Vikundi 156 pekee ndiyo taarifa zake zimepatikana.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameruhusu kuanzia sasa mchakato wa utolewaji wa Mikopo hiyo uendelee baada ya kusimamisha kwa muda wa mwezi mmoja ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza.
Kikao hicho kimewajumuisha Viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwemo Watumishi wa Idara za Fedha na Mipango,Kamati ya Ulinzi na Usalama, na Idara ya Maendeleo ya Jamii na Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.