Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Mhandisi Robert Gabriel ameongoza mafunzo kwa Watumishi wa Halmashauri ya Misungwi yanayohusu namna ya utoaji na matumizi sahihi ya fedha za Mikopo ya asilimia kumi zinazotolewa na Halmashauri kwa Makundi maalum.
Zoezi hilo la Mafunzo linafanyika ikiwa ni maelekezo yake aliyotoa Aprili 25 mwaka huu baada ya kutangaza kusimamisha utoaji wa Mikopo hiyo kutokana na kubainika Halmashauri kufanya ubadhirifu wa fedha wakati wa utoaji wa Mikopo hiyo.
Mafunzo hayo yanayotolewa na timu ya Wataalamu wa masuala ya Miradi na Tathmini,TAKUKURU na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,yamelenga kuwaelimisha sheria na kanuni za namna ya utoaji wa Mikopo hiyo.
Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel amesema fedha hizo za Mikopo ipo ndani ya Ilani ya Uchaguzi kuyalenga Makundi maalum kujikwamua na tatizo la ajira.
"Wilaya hii ya Misungwi ni miongoni mwa zilizopata tatizo la ubadhirifu wa utoaji wa Mikopo, fedha iliyorejeshwa hadi sasa ni Milioni 57 bado Bilioni 4.3" amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la kuzuia rushwa Mkoa wa Mwanza,Stella Bukulu amesema katika uchunguzi wao wamebaini mapungufu mengi kwa Idara zilizohusika na utoaji wa Mikopo hiyo ama kwa kutokujua au uzembe.
Prudence Sempa ambaye ni Mtaalamu wa masuala ya Miradi na Tathmini kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amefafanua Sheria kadhaa kwa Vikundi vinavyotaka fedha za Mikopo.
Washiriki wa mafunzo hayo ni Kamati za fedha na mipango,Wakuu wa Idara kutoka Halmashauri ya Misungwi,pamoja na Watendaji kata wote kutoka ndani ya Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Mhandisi Robert Gabriel anasimamia mafunzo hayo kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza baada ya kubainika ubadhirifu wa fedha za mikopo za asilimia kumi ambazo zimewalenga Makundi ya Vijana,Wanawake na watu wenye ulemavu..
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.