RC MWANZA ASIKILIZA KERO ZA WAMACHINGA,VIONGOZI WA MASOKO NA MINADA MKOANI MWANZA
*Awataka Machinga kufanya biashara kwenye maeneo waliyopangiwa*
*Aaagiza kuwepo dawati la kusikiliza kero za wafanyabiadhara kila Halmashauri*
*Aitaka LATRA kuweka utaratibu wa mizunguko ya mabasi kwenye masoko ili kuwe na muingiliano wa watu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla amekutana leo viongozi wa makundi ya wafanyabiashara kwa lengo la kusikiliza kero zao na kutoa maagizo kumi likiwemo la kuwasisitiza kufanya biashara zao kwenye maeneo waliyopangiwa huku mikakati ya kuboresha maeneo yao ikiendelea kufanyiwa kazi.
Akizungumza na makundi ya wawakilishi hao kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ametoa maagizo likiwemo la kuzitaka Halmashauri zote Mkoani humo kuwa na dawati la kusikiliza kero za wafanyabiashara hao ambalo litasaidia kuzitatua changamoto zinazowakabili za mara kwa mara.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ana uzoefu na changamoto za wafanyabiashara kutokana na kufanya kazi kwenye majiji kadhaa nchini amewaagiza kila Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Maafisa biashara kuweka mpango mkakati wa kuboresha masoko katika maeneo yao.
"Nawaagiza pia LATRA kuhakikisha wanaweka mpango wa mizunguko ya mabasi kupita kwenye masoko yote ili kuwepo na muingiliano wa watu na biashara iweze kufanyika kwa tija, haiwezekani kuwaweka wafanya biashara kwenye maeneo ambayo hakuna muingiliano wa watu, wataishia kuyakimbia masoko wakihofia mitaji yao kukatika, LATRA mzingatie hilo,"CPA Makalla.
Kuhusu miundombinu Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo kwa TARURA kuboresha barabara zote maeneo ya masoko ili kuhakikisha zinapitika kwa urahisi ili shughuli za kupeleka mizigo na wanunuzi zifanyike kwa wepesi.
Aidha, Makalla amewakumbusha Wakuu wa Wilaya kuwa na vikao vya mara kwa mara na wafanyabiashara hao hali ambayo itasaidia kuzitambua kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.
Kuhusu Soko kuu lililopo katikati ya Jiji linalotarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali Disemba mwa mwaka huu, Mhe.Makalla amewahakikishia kipaumbele kitatolewa kwa wafanyabiashara wa awali ambao walikuwepo kabla ya kupisha mradi huo kufanyika.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa rai kwa wafanyabiashara hao kuwa na umoja na kudumisha amani katika shughuli zao na amewaahidi kuwa na vikao nao vya mara kwa mara ili kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa Wilaya yangu Ina jumla ya wafanyabiadhara 12,850 na masoko 15 licha ya changamoto za hapa na pale lakini biashara zao tunahakikisha zinafanyika katika mazingira mazuri," Amesema Mhe.Amina Makilagi,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana.
."Wilaya ya Ilemela tuna jumla ya wafanyabiashara 3500 na masoko 8 yaliyo rasmi na yasiyo rasmi lakini tumekuwa makini kuhakikisha wafanyabiashara hao wanatii bila shuruti miongozo iliyopo,"Mhe.Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.