*RC Mwanza awaongoza Wananchi kutembelea Vivutio vya Utalii Jijini humo*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe Mhandisi Robert Gabriel amewaalika wananchi kufanya Utalii kwenye vitutio vilivyopo Mkoani humo kama Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane, Bismark Rock, Makumbusho ya Bujora na Gunsert House ambapo watawaona wanyama na kujifunza historia ya mambo ya kale.
"Hapa nilipo ni kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saanane ni kisiwa cha kipekee nchini, na kufika hapa kutoka pale mjini ni umbali wa Dakika 5 tu hivyo nawaalika wananchi kuja kuangalia wanyama na vivutio vingine na hata kupumzika na kama hujafika Saasane fikiria mara mbilimbili hapa si pakukosa" Mkuu wa Mkoa.
Pamoja na Utalii uliofanyika leo kwenye vivutio vya Mwanza, amewapongeza watu wote waliokwenda kutalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alhamisi ya Juni 16, 2022 wakitokea Mwanza chini ya Kamati maalumu inayoratibu zoezi la Utambulisho rasmi wa filamu ya ROYAL TOUR
itayofanyika Jumamosi Juni 18, 2022 kwenye viwanja vya Rock City Mall.
"Ni lazima tuweke mazingira rafiki ya utalii hapa, kama tunataka watu waogelee kwenye eneo hili basi tuhakikishe Mamba hawafiki hapa labda kwa kuwawekea uzio maalum wa wavu ili wasifike eneo ambalo watu wanaogelea na uwepo usimamizi watu wasifike kwenye kina kirefu." Mkuu wa Mkoa akiwa kwenye jiwe la Bismark.
"Bwana Gunzert alifika na kujenga nyumba hii na kutawala ukanda wa ziwa, jengo hili la Ofisi na Makazi lilianza kujengwa 1907 hadi 1912 lilikamilika na baada ya kukamilisha ujenzi alianza kutawala makoloni yake na baadae aliwaachia wakoloni wa Kiingereza na baada ya Uhuru tumebaki nalo kama urithi." Afisa Utalii wa Jiji la Mwanza, Sifuni Sospateri.
"Jiwe hili zamani liliitwa Jiwe la Baraka na lilitumika kuabudia lakini walivyokuja wakoloni wa Kijerumani waliita Bismark Rock na waliweka picha ya Chansela wao na waingereza walipokuja waliiondoka picha ile lakini limebaki kuwa na jina hilo, karibuni sana pia kuna bustani nzuri na jiwe hili ndilo lililopo kwenye noti ya Elfu Moja." amefafanua wakati watalii walipofika kwenye Jiwe la Bismark Jijini Mwanza.
Kwa upande wake Mtaalamu wa masuala ya Utalii kutoka Chuo Kikuu cha Mt.Agustino Dktr.Delphine Kessy amesema wapo katika kufanya utafiti wa historia nzima ya nyumba ya Gunzert kuanzia mtu wa kwanza aliyeishi na hatima yao
Mhifadhi mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saanane,Kamishina Msaidizi Eva Malya amesema hifadhi hiyo awali ilikua Bustani ya mtu binafsi ambaye aliishi kisiwani hapo aliyeitwa Mzee Saanane na baadae aliondoka kwenda kisiwa cha Gabalema amnlebainisha kuwa pamoja na hifadhi hiyo iliyotangazwa rasmi 2013 ikiwa na Kilomita za Mraba 2.18, Kanda ya ziwa Magharibi ina Hifadhi 10.
"Mwaka 2021 tumepokea zaidi ya wageni elfu 19 na mwaka huu tayari tumepokea wageni zaidi elfu 21 na tuna imani watazidi malengo ya elfu 22 tuliyojiwekea kwa mwaka na tunashukuru sana Uongozi wa Mkoa kwa ushirikiano mzuri kwenye kuhamasisha utalii hadi kufikia malengo makubwa hivi." Mhifadhi Malya.
Baada ya tukio hilo adhimu Mhe Mkuu wa Mkoa amewakaribisha wananchi kuanzia saa 7 mchana kesho juni 18, 2022 kwenye eneo la Gandh Hall kwa ajili ya naandamano ya furaha na amani ambapo wananchi kwa shamrashamsha wataelekea kwenye viwanja vya Rock City Mall kuangalia filamu ya Royal Tour.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.