_Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel ametoa wito kwa Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala walioko kwenye Serikali kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, Wakala na Taasisi binafsi nchini kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Pili wa Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala utakaofanyika tarehe 15-17 Juni, 2022.
Amesema hayo leo Juni 11, 2022 wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kwa kushirikiana na kamati tendaji ya umoja wa Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala Tanzania ambapo amefafanua kuwa Mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest Jijini Mwanza.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amefafanua kuwa umoja huo ulioanzishwa na kusajiriwa Februari 13, 2018 nchini umesaidia kuwaunganisha Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala kwa lengo la Kubadilishana uzoefu na kuishuri Serikali juu ya namna bora ya usimamizi wa watumishi wa Umma na Sekta binafsi.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa amewapongeza Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala kwa kukutana Mkoani humo huku akibainisha kuwa itasaidia kuongeza ari ya kuchapa kazi na kuonyana kuhusu utendaji kazi wa kuzingatia Weledi wenye tija.
"Uwepo wa Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala zaidi ya 400 hapa jijini ni fursa kwa wafanyabiashara na wadau wa maendeleo na itawapa fursa Maafisa hao kutembelea na kujifunza kwenye vivutio vya kitalii na fursa zilizopo Mkoani Mwanza", amesema.
Mhe Mkuu wa Mkoa amewahakikishia Maafisa hao usalama na amejinasibu hali ya hewa ni tulivu Jijini humo, uwepo wa vyakula bora na amewakaribisha kushiriki kwenye utambulisho rasmi wa Filamu ya Royal Tour itakayofanyika kwenye viwanja vya Rock City Mall siku ya tarehe 18, Juni 2022.
_Mwisho_
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.