RC MWANZA AWATAKA WANANCHI KUENDELEA KUJISAJILI NA KUCHUKUA VITAMBULISHO VYA NIDA
*Asisitiza weledi na Uzalendo kwa Mamlaka kwenye Utambuzi na Usajili wa wananchi*
*Atoa wito kwa wananchi kutunza vitambulisho na kuvitumia kwa mujibu wa sheria*
*Ametoa rai kwa Mamlaka hiyo kuandikisha makundi yenye Uhitaji Maalum*
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo Jumatatu Februari 19, 2024 amezindua ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo na akatumia hafla hiyo kuwataka wananchi kufika kwenye vituo kujisajili na walivyojiandikisha kwenda wakachukue kadi zao kwani zipo tayari.
Balandya amebainisha kuwa tayari NIDA imekamilisha uzalishaji wa Vitambulisho kwa wananchi wapatao 716, 245 na kwamba vingi bado vipo kwenye Ofisi za Serikali za Mitaa na huku wananchi wakiwa na namba tu za kuwatambua jambo ambalo si sahihi hivyo ni wakati sasa wa kuvichukua kwa ajili ya rejea mbalimbali.
Balandya amesisitiza weledi na uzalendo kwa Mamlaka kwenye Utambuzi na Usajili wa wananchi ili waandikishwe wenye sifa kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo na kwamba kwenye utekelezaji wa zoezi hilo wasiliache kundi la watu wenye mahitaji maalum
Vilevile, Katibu Tawala ametoa wito kwa wananchi kutunza vitambulisho na kuvitumia kwa mujibu wa sheria na sio kwa matukio ya uvunjifu wa amani au kutenda makosa ya jinai.
Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mwanza Ndugu Daud Hashim Abdallah ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwani kigezo kikubwa cha utambuzi na usajili ni kwa raia kuwa na Miaka 18 na kwamba Mamlaka hiyo imesajili asilimia 84 ya wenye sifa mkoani Mwanza na zoezi hilo ni endelevu.
Vilevile, ametaja changamoto kadhaa zinazowakabili Mamlaka hiyo kwenye zoezi hilo katika usajili na utambuzi wa wananchi ikiwemo muitikio mdogo wa wananchi katika kuchukua vitambulisho na kupelekea mlundikano wa vitambulisho kwenye ofisi za Serikali za mitaa na vijiji.
"Elimu kupitia vyombo vya habari imeendelea kutolewa na mamlaka kwenye redio na vyombo vingine kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kusajiliwa, kutambuliwa na kuchukua vitambulisho kwenye ofisi za Serikali za mitaa." Amesisitiza Ndugu Abdallah.
Aidha, bwana Abdalah ametaja pia changamoto za wananchi kujisajili zaidi ya mara moja na akatumia wasaa huo kuwataka kuwa na viambata muhimu kwa ajili ya usajili.
Jisajili, tukutambue tukutambulishe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.