Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, amewaagiza wanasayansi wa Maabara za afya mkoani humo kuongeza usimamizi wa ubora wa vipimo mbalimbali katika maabara zote za serikali na binafsi ili kujihakikishia huduma bora.
Mhe. Mhandisi Gabriel pia amewataka wataalamu hao kuongeza kasi ya ukusanyaji wa damu kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya damu kwa wahitaji wote.
Mhandisi Gabriel ametoa maagizo hayo leo Mai, 2 wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya wataalamu wa maabara za afya kimkoa yanayofanyika uwanja wa furahisha hadi Mei , 6 mwaka huu kwa uratibu wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya (MeLSAT)mkoani humo.
"Niwatake wataalamu wa afya mfanye kazi kama timu na kutumia majibu ya maabara (takwimu), muweke mipango endelevu itakayowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbal,"amesema na kuongeza
"Ukusanyaji wa damu umeendelea kufanyika kwa mafanikio ya kiasi cha kufikia asilimia 69 ya malengo ya kukusanya chupa za damu 32,173 kwa mwaka.
Naye Makamu wa Rais MeLSAT, Taifa, Joseph Gimbuya, amesema ili kuboresha afya za watanzania mkazo wa kwanza uwe katika kinga na wa pili katika tiba.
"Lakini tiba isiyo na uchunguzi sahihi wa kiini na aina ya ugonjwa ni kazi bure na huongeza gharama kwa mgonjwa, serikali na taifa kwa ujumla.
" Hivyo tunapotafakari matibabu sahihi yenye gharama nafuu zaidi, matumizi ya maabara ni lazima kwa tabibu ama daktari maana kufanya kazi bila maabara ni sawa na kupiga Ramli au kuwa mganga wa kienyeji,"amesema Gimbuya.
Naye Mwenyekiti wa MeLSAT Mkoa wa Mwanza, Betrand Msemwa, amesema wanachama wote wana ari ya kuwahudumia wananchi wakishirikiana na wanataaluma wengine ili kuhakikisha afya za wananchi zinazidi kuwa bora.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa, ametoa wito kwa wataalamu wa maabara kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuwataka washirikiane ili kulinda taaluma hiyo ili isichafuliwe na watu wachache wenye nia ovu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.