Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, ametoa siku 90 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuwatafuta watumishi 53 ambao wamelipwa mishahara Jumla ya Tshs Milioni 486 kwa mwaka wa fedha 2015/16 wakati wakiwa wameshastaafu.
Mhandisi Gabriel ametoa agizo hilo leo Juni 28, 2022 baada ya kuibuka hoja katika kikao Maalum cha Madiwani cha kujadili Utekelezaji wa Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo Afisa Utumishi wa halmashauri hiyo Mang'oha Maginga alisema awali walikuwa wanadai Tshs milioni 657 kwa watumishi waliolipwa fedha wakiwa wamestaafu na wengine wakiwa wamefariki.
Ndugu Maginga aliendelea kufafanua kwamba baada ya kufuatilia kwa kina watumishi 21 walirejesha Tshs Milioni 111.1 hivyo deni lililobaki ni Tshs Milioni 486 ambazo wanadaiwa watumishi 53 ambao wako hai huku watumishi 21 waliofariki dunia wakiacha deni la shilingi milioni 63.
"Hawa watu wapo katika mfumo wa malipo ya mifuko ya hifadhi ya jamii na wana namba za hundi za malipo hivyo kutokuwafualia kwa kipindi chote hicho ni uzembe wa hali ya juu yaani haiingii akilini mnakuja kuwabaini leo kwenye kikao, sasa nahitaji ndani ya siku 90 fedha hizo za Umma zirudi." Mhandisi Gabriel.
Baada ya kuibuka hoja ya kudaiwa zaidi ya Tshs Bilioni 1 zilizokopwa kutoka kwenye Akaunti ya Amana, Mhe Mkuu wa Mkoa amewaagiza Halmashauri hiyo kuacha tabia ya kukopa fedha na badala yake amewataka kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili kujiendesha kutokana na Mapato ya Ndani.
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani amefafanua kuwa kwa hesabu za mwaka wa Fedha 2020/21 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imepata Hati Inayoridhisha.
Mkutano Maalumu wa kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG katika halmashauri ya wilaya Ukerewe umehitimisha ziara ya Mhandisi Gabriel ya kujadili hoja katika Halmashauri zote za mkoa wa Mwanza zilizoanza juni 20 mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.