Maonesho ya Nanenane Mkoani Mwanza yamefungwa rasmi leo agosti 08, 2022 huku rai ikitolewa kwa washiriki hao kutumia Elimu waliyoipata kutoka kwa wadau mbalimbali wa Kilimo na mifugo kama njia ya kuzidi kuongeza tija kwenye mazao na kuboresha shughuli zao.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella katika hotuba yake ya Ufungaji kwenye Viwanja vya Nyamhongolo amesema kwenye maonesho hayo kuna fursa za kuonana na Wataalam mbalimbali kuanzia Kilimo na masuala ya fedha ambao watamsaidia mkulima au mfanyabiashara kufanya kazi kwa ufanisi.
"Haya ni maonesho yangu ya kwanza kushiriki nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita nimeyazungukia mabanda na kushuhudia fursa nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zitainua uchumi wa washiriki." Mkuu wa Mkoa Geita
Mhe. Shigella amebainisha kuwa, hakuna sababu ya mfugaji kujivunia wingi wa Ng'ombe wakati hawamnufaishi ipasavyo kutokana na kukosa ushauri wa kitaalamu hivyo huu ni wakati wa kubadilika.
Akimkaribisha katika ufungaji huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima amesema kuna kila sababu ya kuyaboresha maonesho hayo hasa baada ya kushuhudia hamasa kubwa ya wananchi na washiriki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya maonesho ya Nanenane Mkoa Emil Kasagara amebainisha maonesho hayo yamekuwa na muitikio chanya kila mwaka kutokana na maandalizi bora wanayofanya.
Kwa upande wa washindi wa zawadi kwa Washiriki Wilaya ya Magu imeonesha kuibuka kimasomaso kutokana na zawadi nyingi kwenda kwa Washiriki kutoka wilayani humo.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yameshirikisha Mikoa ya Geita,Kagera na mwenyeji wao Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.