Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewahakikishia wazee mkoani humo kuwa Serikali itaendelea kuboresha maisha yao kupitia huduma bora za jamii kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.
Amebainisha hayo leo jumatano disemba 28, 2022 kwenye mkutano wake na Umoja wa wazee Mkoa wa Mwanza uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa ukiwakutanisha wazee hao na Maafisa Ustawi wa jamii kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wazee.
"Serikali ya Rais Samia inawathamini sana wazee na Mkoa wetu unahitaji sana busara zenu na ndio maana tupo na Mganga Mkuu hapa ambaye anahakikisha mnapata huduma bora za Afya na hata Elimu bora kwa vijana na wajukuu zenu, Maji safi na salama pamoja na pembejeo za kilimo." Amesema Malima.
Vilevile, ametoa wito kwa wazee kuboresha sifa na masharti ya kujiunga na chama hicho ili waweze kupata wanachama hodari zaidi katika kuwasemea na wenye uwezo wa kubuni miradi itakayowainua kwenye uimarishaji wa huduma za kijamii.
Halikadhalika, ametumia wasaa huo kuvipongeza vyombo vya Ulinzi kwa kuimarisha Usalama kwa wananchi mkoani humo na kufanya wananchi waweze kuishi kwa furaha na amani wakati wakiendelea kwa shughuli zao uzalishaji.
Mwenyekiti wa wazee Mkoa wa Mwanza, Charles Masalakulangwa amesema wamefungua akaunti maalumu ya chama cha wazee mkoani humo ili kukiimarisha chama hicho chenye lengo la kulizungumzia kundi hilo ili liweze kustawi zaidi.
Katibu Msaidizi wa Umoja wa wazee Mkoani humo, Mzee John Mganga amesema umoja huo unaipongeza serikali ya awamu ya Sita kwa Utekelezaji wa Miradi ya kimkakati na kwa kipekee wamempa pongezi Rais Dkt. Samia kwa kuvitangaza vivutio vya Utalii kwa kupitia filamu ya Royal Tour.
Mzee Paulo Sospeter ametoa rai kwa Serikali kusimamia Mapato yatokanayo na machimbo ya dhahabu kwenye kata ya Mpamwa wilayani Kwimba ili yasipotee bali yawe manufaa kwa wananchi kupitia kuliingizia Taifa mapato halali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.