RMO MWANZA ASISITIZA MLO KAMILI NA UFANYAJI WA MAZOEZI KWA WAKATI
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewasisitiza Watumishi wa umma na Wananchi kuzingatia mlo kamili na kufanya mazoezi kwa lengo la kuboresha afya na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambikiza yanaongezeka kwa kasi nchini.
Dkt. Lebba ameyasema hayo asubuhi ya leo tarehe 22 Machi, 2025 alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mara baada ya kuhitimisha matembezi ya kila jumamosi ya tatu ya mwezi kwa watumishi.
Mganga Mkuu amebainisha kuwa mazoezi ni sehemu muhimu sana katika maisha ya binadamu kwa lengo la kuimarisha Afya na kuwa imara muda wote na kwamba yanasaidia mwili kupambana na bakteria na vimelea vyemelezi vya maradhi mbalimbali kwa kuupa kinga imara mwili.
“Mazoezi ni sehemu muhimu sana ya kuimarisha mwili na Afya yako, yanasaidia kuuufanya mfumo wa mwili kuweza kufanya kazi vizuri, husaidia pia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, kupunguza msongo wa mawazo na changamoto nyingine katika miili yetu”. Amesema.
Aidha, ameongeza kwa kuwataka wananchi na watumishi kuzingatia mlo kamili pamoja na mazoezi Ili kuweza kuruhusu mwili kuepuka changamoto za maradhi kama kisukari na saratani, magonjwa ya moyo, yote hayo yana gharama kubwa sana na yana zuilika kwa mazoezi na kubadilisha mtindo wa maisha hususani kwenye kuzingatia lishe Bora na mlo kamili.
“Muhimu tuhakikishe tunapata mlo kamili, lishe bora, mazoezi, kunywa maji mengi na kula matunda Ili kuweza kusaidai mfumo wa mwili Ufanye kazi yake kwa ufasaha”. Amesisitiza Mganga Mkuu.
Kwa upande wake mshiriki wa matembezi hayo Elizabeth lupindo ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa mwanza kwa kuanzisha utaratibu huo wa mazoezi kwa maana unawapa hamasa, nguvu na hata kupunguza vitambi kwa baadhi yao, huku akizidi kuomba matembezi hayo yawe endelevu.
Matembezi hayo maalumu ya kuzuia magonjwa yasiyo ambukiza kwa watumishi na Wananchi yanalenga kuimarisha afya, yalizinduliwa rasmi Januari 18, 2025 hivyo ni mwendelezo na hufanyika kila jumamosi ya tatu ya mwezi .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.