RS MWANZA WATEMBELEA JNHPP, WAIPONGEZA SERIKALI KWA MRADI WENYE SULUHU YA UMEME NCHINI
Leo tarehe 28 Machi, 2025 watumishi takribaki 30 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wamefanya ziara katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kufika katika mradi wa kimkakati wa kufua umeme kwa chanzo cha maji wa Julius Nyerere (JNHPP) mkoani Pwani.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu Bw. Henry Mwaijega amesema mradi huo una tija sana kwa maendeleo ya uchumi wa watanzania kwani Megawati 2115 za umeme zinazozalishwa hapo zinakidhi mahitaji ya nchi na ziada hivyo zitawasaidia kujiimarisha kwenye shughuli za kujitafutia ridhiki.
Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. Mangabe Mnilago ametoa wito kwa TANESCO kuhifadhi mazingira na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa mradi huo na kwamba maji yaliyokusanywa hayataathiri makazi yao kwa mafuriko kwani yanaratibiwa.
Kaimu Mhandisi Mkazi wa Mradi wa JNHPP Mhandisi Luteganya Kamugenyi amesema bwawa hilo lenye mita 133 linajumuisha mageti 7 ya kuruhusu na kuzuia maji ambapo mitambo 9 ya kufua umeme yote imewashwa na kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imedhamiria kuwapatia wananchi wake nishati ya umeme kwa gharama nafuu kwani chanzo cha maji ni rahisi kulinganisha na vyanzo kama joto ardhi, upepo, jua, mafuta na hata gesi.
Katika nyakati tofauti watumishi hao wamempongeza mratibu wa safari hizo takribani 4 tangu mwanzoni mwa mwezi Februari Bw. Paul Cheyo ambapo wamesema wamejionea vivutio mbalimbali kama wanyama pamoja na uoto wa asili ambao Serikali imekuwa ikihifadhi kwa manufaa ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.