SAMIA TEACHER'S MOBILE CLINIC YAZINDULIWA MWANZA
Kampeni ya Samia Teacher's Mobile Clinic imezinduliwa rasmi Mkoani Mwanza ikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto na kero zinazowakabili walimu Mkoani Mwanza na nchi nzima kiujumla.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Loreto Wilayani Ilemela leo Februari 22, 2025 na kuhudhuriwa na Walimu kutoka Wilaya za Ilemela, Magu na Ukerewe.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amesema Serikali Mkoani humo inaendelea na jitihada za kutatua changamoto za walimu ambapo kila siku ya jumanne Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imekuwa ikisikiliza kero za wananchi mbalimbali wakiwemo Walimu.
“Tusiishie hapa tu, hata kliniki itakapokwisha nawashauri mfike Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ile ni yenu na iko wazi wakati wowote ule”.
Halikadhalika, Katibu Tawala amewahakikishia Walimu hao kuwa yeye kama Kiongozi wa Utumishi katika Mkoa wa Mwanza atahakikisha anasimamia haki na uwajibikaji kwa Walimu na hatasita kumchukulia hatua yoyote yule atakaekwenda kinyume na utaratibu, miongozo na kanuni za kiutumishi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwl. Suleiman Komba, amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia walimu wote wenye changamoto na amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuruhusu na kukubali kampeni hiyo ikawafikie walimu.
Sambamba na hilo amewataka Walimu hao kutimiza wajibu wao kwa kila Mwalimu kusimamia somo alilopewa kikamilifu kama ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia alivyoruhusu walimu hao kusikilizwa na kutatauliwa changamoto zao.
Mwanza unakuwa Mkoa wa 19 kufikiwa na kampeni hiyo tangu kuzinduliwa kwake aidha kliniki hiyo kwa siku ya kesho tarehe 23 Februari 2025 inatarajiwa kuendelea katika Wilaya za Kwimba, Misungwi na Nyamagana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.