*SAUT wamkumbuka Hayati Mkapa kwa kutoa Mikopo Wanafunzi Vyuo Binafsi*
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT) Profesa Costa Ricky Mahalu, amesema Hayati Benjamin William Mkapa atakumbukwa kwa kushawishi sekta binafsi kuwekeza nchini hasa katika maswala ya elimu ya juu hali iliyosaidia kuongeza kiwango kikubwa cha wahitimu wa vyuo vikuu nchini.
Akizungumza Chuoni hapo leo Novemba 12, 2022 kwenye uzinduzi wa Kigoda cha Utafiti cha Benjamin Mkapa, Profesa Mahalu amesema Mkapa aligusa maisha ya watanzania wengi kwani akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali ilianza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wenye sifa waliokuwa wakisoma vyuo vikuu binafsi mwaka 1995.
"Hayati Mkapa aligusa sana sekta binafsi hasa katika elimu leo hatuwezi kufurahia tukiwa na vijana wengi waliohitimu vyuo vikuu bila kumtaja, mtakumbuka kabla ya mwaka 2005 Serikali ilikuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya serikali peke yao, hivyo vijana wengi wenye sifa ya kusoma vyuo vikuu walikosa fursa kutokana na wazazi au walezi kushindwa kumudu gharama.
"Mwaka 2001 alipokuja hapa chuoni SAUT kwenye mahafali ya kwanza akiwa mgeni rasmi wakati huo alikuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi wenye sifa wataanza kupata mikopo kabla hajatoka madarakani, wakati huo SAUT ilikuwa na wanafunzi chini ya 400 leo tunawanafunzi zaidi ya 16,000, mafanikio hayo yametokana na mikopo inayotolewa na Serikali,"amesema Balozi Profesa Mahalu.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Uganda, Profesa John Mugisha, amesema Hayati Mhe. Mkapa alikuwa ni kiongozi anayesikiliza watu wengine wa kada mbalimbali hata kama wanatofautiana itikadi pia alikuwa tayari kufanya kazi na watu wanaotoka mataifa ya nje.
Mkuu wa Idara ya Falsafa kutoka Chuo cha SAUT, Padri Dkt.Innocent Sanga, amemuelezea Hayati Mhe.Mkapa kwamba alikuwa mchambuzi na mkosoaji, hakupenda ubaguzi alikuwa anapenda kusali,alikuwa anasikiliza ushauri na kufanya maamuzi makini bila kuyumba.
"Alikubali kushindwa kwa hoja alikuwa na fikra yakinifu na bunifu, washauri wabaya enzi za uongozi wake hawakuwa na nafasi kwake,"amesema Padri Dkt. Sanga.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mchumi aliyebobea amesema, Hayati Mhe.Mkapa ameacha alama ambayo inagusa mioyo, macho na masikio ya vizazi vya sasa na vijavyo kwani alishika madaraka kukiwa na mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa lakini aliyatengenezea misingi na kuyasimamia
kwani aliamini katika utekelezaji wa uchumi wa ubia.
"Nipende kuwahakikishieni kuwa yapo mambo mengi kwenye Serikali ya awamu ya sita ya Mhe.Samia Suluhu Hassan ambayo ni mwendelezo wa yale aliyoyayaanzisha Mhe. Hayati Mkapa ikiwemo bima ya afya ambayo sasa Serikali iko katika mchakato wa kuhakikisha kila Mtanzania anufaika nayo.
Akimzungumzia Hayati Mhe.Mkapa, Balozi Profesa Ombeni Sefue, ambaye alikuwa mzungumzaji Mkuu kwenye uzinduzi huo amesema alikuwa akiheshimu haki ya kuishi na hilo alilithibitisha kwa kutotia saini ya watu waliohukumiwa kunyongwa ili wanyongwe.
Pia alitumia muda wake mwingi kusoma vitabu na majarida badala ya kukaa kijiweni na kuongea mambo yasiyo ya faida kwa jamii maana aliamini
kwamba vitabu ni muhimu katika kurutubisha akili nafsi, moyo na roho ya mwanadamu.
Balozi Profesa Sefue ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Viongozi Dar Es Salaam ameendelea kumuelezea Hayati Mhe. Mkapa kwamba alikuwa ni mwaminifu ambapo alipenda kusema ukweli na uwazi, mara kwa mara alisema bora achukiwe kwa kusema ukweli kuliko kupendwa kwa kudanganya.
Naibu Mkuu wa Skuli ya Sheria - Taaluma Zanzibar, Wakili Msemo Mavare amesema tasnia ya sheria itamkumbuka Hayati Mhe. Mkapa kwa mchango wake katika utawala wa sheria kwani ndiye Rais mstaafu pekee Afrika aliyekwenda mahakamani kutoa ushahidi kumtetea Profesa Costa Ricky Mahalu wakati anashtakiwa, alikuwa tayari kuhojiwa ili haki itendeke.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.