SERIKALI IMETENGA BILIONI 4 KUJENGA HOSPITALI YA MKOA YA RUFAA UKEREWE: WAZIRI UMMY
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imenuia kuondoa adha ya matibabu kwa wakazi wa Ukerewe na visiwa vya jirani kwa kutenga shs bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya mkoa ya Rufaa wilayani humo.
Akitoa taarifa fupi leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya ukimwi Waziri Ummy amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kwa vitendo kuwaletea wananchi maendeleo ikiwemo kuiboresha sekta ya afya.
"Ndugu mwenyekiti wa kamati nimesimama hapa kutoa taarifa fupi ya Serikali, usumbufu wa matibabu na hata vifo kutokakana na jiographia ya Ukerewe sasa basi, naomba fedha zitakapofika Ofisi ya mkuu wa Mkoa mfanye usimamizi mzuri ili mradi huu wa ujenzi ukamilike kwa wakati na uwe na tija kwa wananchi", amesisitiza Mhe. Ummy
Kuhusu suala la upungufu wa watumishi zaidi ya elfu kumi kwenye sekta ya afya, Waziri Ummy ameziagiza Halmashauri zote mkoani humo kutumia mapato yao ya ndani kuwaajiri watumishi kwa mikataba wakati utaratibu wa ajira rasmi kutoka Serikali kuu ukiendelea kufanyika.
Waziri Ummy pia amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa usimamiaji mzuri wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na kuhimiza utoaji wa elimu uzidi kuzingatiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema Mkoa huo umepokea jumla ya shs bilioni 48 ambazo ni gharama ya miradi ya afya na akaahidi kutaendelea kuisimamia ili iwe na tija kwa wananchi.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya ukimwi ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki Mhe. Stanslaus Nyongo amesema jukumu la kamati yake ni kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa na pia kuishauri Serikali mpango sahihi wa kuwaletea maendeleo wananchi.
"Hospitali ya Sekou Toure tangu ilipoanza kuwa ya rufaa imezidi kupiga hatua kwa kutoa huduma bora na za kibingwa hasa baada ya Serikali kuzidi kuiboresha.
"Mhe Mwenyekiti wa kamati hospitali ya Sekou Toure sasa hivi tunatoa huduma za kusafisha damu pia Serikali imewasomesha Madaktari 17 tabibu za kibingwa lengo likiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi", Dkt. Bahati Msaki, Mganga Mfawidhi Sekou Toure.
Kamati hiyo ya Bunge itahitimisha ziara yake alhamisi ya hii kwa kutembelea Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Bugando.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.