SERIKALI INAKAMILISHA TARATIBU ZA KUMPATA MKANDARASI WA UJENZI WA BARABARA SENGEREMA-NYEHUNGE : RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi wa Wilaya ya Sengerema kuwa na subira wakati Serikali ikikamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga barabara ya Sengerema -Nyehunge kwa kiwango cha lami.
Amebainisha hayo leo Juni 10, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo katikati ya mji huo ambapo ulikua wa muitikio mkubwa wa wananchi waliokua na kiu ya kumsikiliza kiongozi huyo wa Mkoa.
Amesema, awali Serikali ilitangaza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo
yenye umbali wa takribani KM 50 na kwamba alipatikana mjenzi ambaye alitumia vyeti vya kughushi na kusababisha kupewa kazi wakati hakuwa na uwezo wa kutekeleza na kupelekea Serikali kuwaondoa na iko mbioni kuwachukulia hatua kwa udanganyifu.
"Serikali inayo nia ya dhati ya kujenga barabara ya Sengerema hadi Nyehunge kwa kiwango cha lami na sasa ipo kwenye mchakato wa kumpata mkandarasi mzuri wa kufanya mradi huo baada ya kumuondoa aliyepatikana awali ambaye amebainika kutokua na uwezo"
Vilevile, amewataka vijana kuchapa kazi na kuacha tabia ya kuketi kwenye vijiwe kwani wanasababisha kulirudisha nyuma Taifa kimaendeleo na badala yake wanapaswa kujibidiisha kujitafutia maendeleo kwa kufanya shughuli halali.
Vilevile, Mhe. Mtanda amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo ndani ya siku 14 kumlipa fidia Bi. Salome Kazungu ambaye mwaka 2017 Halmashauri ililitwaa eneo lake ili kulitumia kama eneo la kuzikana na endapo watashindwa kufanya hivyo atalirejesha kwa mmiliki huyo kwani hajapata haki yake kwa mujibu wa sheria ya ardhi na akatumia wasaa huo kuwataka sekta ya ardhi kushughulikia kero na migogoro.
Mhe. Hamis Tabasam, Mbunge wa Sengerema ametumia jukwaa hilo kumpongeza Rais Samia kwa kuwaletea miradi lukuki ya maendeleo huku akibanisha kuwa kwa sasa kuna shule za Msingi kwenye kila Kijiji na kwamba huduma za maji safi zimeimarika.
Aidha, Mhe. Tabasam amesema kuhusu mikopo kwa wananchi kutoka kwenye fungu la asilimia kumi kutoka fedha za mapato ya ndani tayari zimetengwa zaidi ya Shilingi milioni 300 ambazo zinasubiri utaratibu tu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ili zianze kukopeshwa kwa makundi husika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.