SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA SEKTA BINAFSI NA ITAENDELEA KUWABORESHEA MIUNDOMBINU: RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda ameendelea na kukutana na makundi mbalimbali kwa lengo la kutambuana ambapo leo Mei 13,2024 amekutana na Maafisa Usafirishaji maarufu kama bodaboda kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela na kuwaambia Serikali inatambua mchango wa Sekta binafsi na inaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya miundombinu ili wafanye kazi zao vizuri.
Akizungumza na Maafisa hao eneo la Buhongwa Wilayani Nyamagana, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Sekta binafsi na rasmi zote zinachangia pato la taifa hivyo Serikali imekuwa na wajibu wa kuhakikisha wanafanya kazi zao katika mazingira rafiki huku wakifuata miongozo yote ya sheria za nchi.
"Ndugu zangu Maafisa Usafirishaji nimewafuata hapa leo lengo ni kutambuana nina karibu mwezi sasa tangu nihamishiwe hapa,rai yangu kwenu kuweni mabalozi wazuri wa amani na kuzingatia sheria zote za barabarani ili kuepusha ajali,kero zenu nazitambua nawahakikishieni zitapatiwa ufumbuzi," Mkuu wa Mkoa.
Mtanda amebainisha Maafisa Usafirishaji hao wanafanya shughuli zao ili kuhudumia familia zao na siyo vinginevyo, hivyo hayuko tayari kusikia kuna aina yoyote ya uonevu dhidi yao au kuwakwamisha kutekeleza majukumu yao, amewahakikishia pia kuwawekea mazingira mazuri ya kukopeshwa.
Aidha amewataka Maafisa hao kufanya kazi kwa kuzingatia miiko ya kazi zao na Serikali haitakuwa tayari kuwaona baadhi yao wakijihusisha na uvunjifu wa amani.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa barabara ya Sawa haipitiki tunaomba sana tusaidie ifanyiwe marekebisho maana vyombo vyetu vinachakaa kwa haraka kutokana na hali hiyo," Bosco Yohane,Afisa usafirishaji
Akiwa Wilayani Ilemela na Maafisa Usafirishaji wa pikipiki za miguu mitatu (Bajaii) amesema anatambua mvutano uliopo baina ya Bajaj na daladala na maeneo ambayo hawaruhusiwi kuingia na amewahakikishia changamoto hiyo itapatiwa ufumbuzi akishirikiana na wakuu wa Wilaya na sekta nyingine kama LATRA, TARURA na Taasisi za Bima.
"Ndugu zangu katika mkutano huu sina mengi zaidi ya kufahamiana ili mkaendelee na shughuli zenu, nawahakikishieni ushirikiano kati ya Serikali nanyi zingatieni amani na usalama na epukeni kutumika vibaya muwe wa kwanza kuwadhibiti wenzenu ambao mtaona wanakwenda kinyume na Sheria za nchi," Mkuu huyo wa Mkoa.
Mhe. Mtanda amesema Mwanza imeingiziwa Shilingi Bilioni 1.2 za mikopo kwa yale makundi maalum wakiwemo vijana, utaratibu utafanyika ili waweze kunufaika na amepongeza pia Afisa Usafirishaji kutoka Jeshi la Polisi (RTO) Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sunday Ibrahimu na kumtaka kuongeza bidii ili Maafisa Usafirishaji hao wafanye kazi zao vizuri bila bugudha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.