SERIKALI ITAENDELEA KUTOA VIFAA TIBA ILI KUBORESHA SEKTA YA AFYA:RC MTANDA
Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu na Utawala Bw.Daniel Machunda amefunga mkutano wa umoja wa Wahandisi na mafundi sanifu vifaa tiba kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwahakikishia Serikali ya awamu ya sita itaendelea kutoa ushirikiano na marafiki wa maendeleo ili kuboresha sekta ya afya.
Akizungumza leo Novemba 21,2024 na washiriki wa mkutano huo wa saba wa siku mbili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye ukumbi wa mikutano Malaika wilayani Ilemela Jijini Mwanza,Machunda amesema Serikali inatambua mchango wa Taasisi mbalimbali zinazojihusisha na afya hivyo ushauri na mapendekezo yote yaliyoazimiwa kwenye mkutano huo yatafanyiwa kazi.
"Ndugu washiriki awali ya yote nichukue nafasi hii ya kumshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kuboresha sekta hii hapa nchini,mfano mzuri ni hapa Mwanza miradi mingi ya afya tunayo na ipo katika hatua nzuri,"Machunda.
Ameongeza kuwa mkutano huo umewajumuisha Wahandisi wa vifaa tiba kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na hatua kubwa ya utolewaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa vyama vya Wahandisi na mafundi sanifu wa vifaa tiba Afrika Mashariki (FEAHEA) Mhandisi Costica Witonze amebainisha siku mbili za mkutano huo wameangalia changamoto, wamejadiliana na kupendekeza mkakati mwafaka wa kuboresha sekta hiyo hasa eneo la vifaa tiba.
"Ndugu mgeni rasmi tunatambua umuhimu wa sekta hii,ingawa zipo changamoto mbalimbali za kifedha kwa nchi za Jumuiya hii katika kufikia malengo tuna imani baada ya mkutano huu tutakuwa na maazimio chanya yatakayosaidia kusonga mbele",Rais wa Jumuiya ya Wahandisi.
Mkutano huo uliobeba kauli mbiu ya "Upatikanaji wa hewa tiba ya Oksijeni na Usimamizi wa vifaa tiba ni chachu ya huduma bora za afya",nchi ya Rwanda watakuwa wenyeji wa mkutano ujao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.