SERIKALI ITAENDELEA KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI - RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwaletea programu katika kila sekta ili waweze kuwekeza mitaji na kukua kiuchumi hususani shughuli za ujasiriamali.
Amebainisha hayo leo Novemba 15, 2024 wakati akifungua mkutano wa uwezeshaji wanawake kiuchumi uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa uliolenga kutambulisha programu ya 'Imarisha Uchumi na Mama Samia'.
Akifafanua hilo Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema Mwanza imekua shuhuda wa juhudi hizo kama vile ukopeshaji wavuvi boti za kisasa za zaidi ya Bilioni 1 kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi kupata tija kwenye uvuvi na mazao yatokanayo na ziwa victoria.
Ameongeza kwa kusema kuwa ndani ya Mkoa huo kuna zaidi ya Vikundi 35 vya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ambavyo vimekopeshwa zaidi ya bilioni 4.4 na Benki ya Maendeleo ya kilimo (TADB) kwa ajili ya kuwainua kimtaji na kuwaondoa kwenye uvuvi wa zamani na kufuga kisasa.
"Mradi wa vijana wa unenepeshaji mifugo kwenye shamba letu la Mabuki umewawezesha vijana 35 kupata ujuzi wa ufugaji wenye tija na wameshahitimu na hivi karibuni Serikali itawapatia vitalu kule Kitengule kwa ajili ya kufanya ufugaji." Amefafanua Mhe. Mtanda.
Naye, Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Bi. Beng'i Issa amesema baraza hilo limelenga kuhakikisha kuwa sera ya uwezeshaji inatekelezwa vema nchini kwa kukusanya maoni kwa wadau wake wote nchi nzima ili kupata dira.
Vilevile, ameongeza kuwa wawapo Mikoani wanatoa fursa kwa watanzania kutoa maoni na kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao moja kwa moja na kwamba kwa sasa wapo kwenye kubaini shughuli za kiuchumi za kila eneo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.