SERIKALI KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA KIMATAIFA KUIMARISHA UPATIKANAJI MAJI MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 20 septemba, 2024 amewapokea na kufanya mazungumzo mafupi na viongozi kutoka Benki ya uwekezaji ya Ulaya (European Investiment Bank- EIB) wenye nia ya kuboresha usambazaji maji kutoka chanzo cha Butimba.
Akizungumza na ujumbe huo uliofika kufanya upembuzi wa kukidhi vigezo vya kupata fedha kwa ajili ya mradi wa awamu ya pili wa Usambazaji Maji, Mhe. Mtanda amewashukuru kwa kushirikiana na serikali kwenye sekta hiyo muhimu.
Amesema, chanzo cha Capripoint kilichokua kikizidiwa na ongezeko la watu na kusababisha changamoto ya maji Mkoani humo ndipo serikali ikajenga chanzo kipya cha Butimba hivyo usambazaji ambao EIB unatarajia kuufanya umekuja muda sahihi kabisa.
"Mwanzo ina watu zaidi ya milioni 3 na hasa mjini ndio kuna ongezeko kubwa zaidi, tukiwa na maji ya kutosha na usambazaji wa uhakika tutakua na uhakika wa Afya bora kwa jamii na kuongeza thamani ya uchumi wa mkoa kupitia shughuli za uzalishaji." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Bi. Nelly Msuya amesema mradi huo (Phase 2 na 3) utaimarisha upatikanaji wa maji kwa kusambaza mtandao kwa kilomita 700 kwenye wilaya za Ilemela, Nyamagana, Magu na Misungwi.
Naye, Afisa Mikopo wa EIB kwa Ukanda wa Afrika Bi. Lily Munyigi amesema wana furaha kufanya kazi na Serikali tulivu ya Tanzania na kwamba wanafurahia ushirikiano mkubwa uliopo baina ya pande hizo mbili na kwamba jumuiya hiyo inajivunia amani iliyopo nchini kwani inaruhusu uwekezaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.