SERIKALI MBIONI KUUNDA BARAZA LA KUWASAIDIA VIJANA KATIKA SANAA:WAZIRI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania chini ya ofisi yake imejapanga kuunda baraza la vijana ambalo litawasaidia katika kupunguza changamoto za ajira na kusaidi katika upatikanaji wa fursa za kiuchumi.
Amesema hayo Septemba 26, 2024 wakati akizungumza na viongozi wa makundi mbali mbali ya Vijana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kuwahamasisha Vijana kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.
Amesema Wizara yake inakwenda kufanya kazi na wizara mbali mbali ili kuhakikisha wanatengeneza fursa za kisanaa kwa vijana ili waweze kuzitangaza na kuzionesha kazi za sanaa zinazofanywa na vijana.
"Baraza hili la vijana litakapoundwa ndiyo litakwenda kuwa mwarobaini kwa vijana katika kuendeleza mambo yao na kupitia vituo tamizi ambavyo vitawekezwa baadhi ya maeneo". Amesema Mhe. Kikwete.
"Tunakwenda kufanya kazi na Wizara ya Michezo, Wizara na Utalii ili kufaidisha kazi za wasanii na kuwasaidia wasanii kuondoka katika wimbi kubwa la umasikini". Amesema Mhe. Kikwete.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Ofisi yake inajipanga ili kuweza kuwasikiliza wasanii wa Mkoa huo na kuweka mikakati ya kuiendeleza sanaa yao.
"Nimeisha waelekeza watu wangu hapa wanaosimamia michezo kutengeneza ratiba ya kukaa na makundi mbali mbali ya wasanii ili Mkuu wa Mkoa aweze kujua na aweze kuwa na mchango katika makundi yenu" Amesema Mhe. Mtanda.
Sambamba na hayo Mhe. Mtanda amewataka Vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.