SERIKALI MKOA WA MWANZA KUENDELEA KUWAUNGA MKONO WAFANYABIASHARA WAKUBWA NA WADOGO
Serikali Mkoa wa Mwanza imedhamiria kuwaunga mkono Wafanyabiashara mbalimbali Wakubwa na wadogo wanaopatikana katika Mkoa huo kwa kuwa Serikali ya Rais Samia inathamini mchango wao katika kukuza uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuitambulisha Kampuni ya AI Mansour Auto Tanzania, Isuzu East Africa na MRC Motors ambao ni wauzaji wa magari mapya ya Isuzu Jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa amesema Serikali ya Rais Samia imeimarisha uchumi na usalama kwa hali ya juu na amewatoa hofu Wafanyabiashara hao kuwa na amani hata wakileta magari zaidi ya mia tano Mkoani Mwanza wajue kuwa yapo sehemu salama.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesema kampuni hiyo ya Isuzu kuja kuwekeza katika Mkoa wa Mwanza hawajafanya makosa kwani ni mkoa wa kimkakati na wenye idadi kubwa ya watu ukiwa pia ni kitovu cha uchumi wa Mikoa 7 ya Kanda ya Ziwa.
“Nyie wenyewe kupitia Bwana Ochieng mmekiri kwamba hata mteja wenu wa kwanza alitoka Mkoa huu kwa iyo mnapofanya Mwanza kama sehemu yenu ya biashara nyie ni wachumi wazuri na mnafahamu kuhusu soko lilipo”.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa Wananchi kutembelea ofisi za Isuzu Mwanza ili waweze kupata huduma za magari na sasa si lazima kwenda Dar es Salaam yameletwa hapa na kizuri zaidi wanauza magari toleo la kwanza na sio yale yaliyotumika.
Naye Mkurugenzi wa Wateja kutoka Kampuni ya Isuzu Afrika Mashariki Bw. Kelvin Ochieng amesema Isuzu ni kampuni inayothamini wateja wake na kwa miaka 5 tangu kuanzishwa kwake wameshauza magari zaidi ya 1200.
Aidha amesema kwa hapa Mwanza wamekuwa wakiungwa mkono na wadau wengi kutoka makampuni na mashirika mbalimbali ya serikali na kuwataka Wafanyabiashara na wadau kuwaunga mkono.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.