**Serikali yaahidi kuendelea kuboresha mazingira ya Wauguzi nchini.*
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameahidi Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa Wauguzi nchini kutokana na kutambua mchango wao katika Sekta ya afya nchini.
Akizungumza kwa niaba yake katika hafla ya ufungaji wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wauguzi nchini TANNA kwenye ukumbi wa Malaika Resort, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndg.Balandya Elikana amesema Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele cha bajeti Sekta ya afya kwa kuboresha huduma zote kwa ujumla yakiwemo mazingira ya Wauguzi.
Amesema siyo rahisi kutatua changamoto zote kwa mara moja zinazowakabili kada hiyo,lakini kadiri bajeti inaporuhusu kipaumbele kitawekwa lengo likiwa kuboresha kwa ujumla Sekta ya afya nchini
"Nimesikia katika risala yenu baadhi ya changamoto zinazowakabili,yale ya ngazi ya Mkoa tutayafanyia kazi na yale yaliyo juu ya uwezo wetu yatafikishwa TAMISEMI ili yapatiwe ufumbuzi",amesema Mtendaji huyo wa Mkoa
Aidha amewakumbusha Wauguzi hao Mkutano huo wa siku tano uliofanyika Mwanza umeambatana na makongamano mbalimbali ya Kisayansi,wayatumie kama chachu ya kuongeza ufanisi wa kazi watakaporudi makazini.
"Kipaumbele chetu sasa ni ubora wa huduma,wakati Serikali ikizidi kuwekeza katika Sekta ya afya,Wauguzi nao wanaendelea kupatiwa mafunzo mbalimbali yakilenga staha,heshima na maadili ili wateja waendelee kupatiwa huduma bora,hadi sasa Wauguzi 2500 wamepatiwa mafunzo hayo",Saturin Mwanangwa,Mkurugenzi wa huduma na uuguzi Wizara ya Afya.
"Licha ya mazingira yenye changamoto kwa Kada hii ikiwemo kutoa huduma kwa wateja wengi,lakini tutaendelea kusimamia kiapo chetu cha kuwa watumishi wenye weledi,"Alexander Baluya,Rais wa TANNA.
Ufungaji huo umekwenda pamoja na Maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani inayofanyika kila Mei 12 yaliyokwenda pamoja na kurudia kiapo kwa Wauguzi hao akikumbukwa mwanzilishi wa huduma za uuguzi na ukunga Duniani,Florence Nightingale raia kutoka Italia.
Mara baada ya kutoka katika ufungaji huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amemtaka Mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano na Uokozi Ziwa Victoria chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kumaliza mradi huo kwa wakati na kuzingatia ubora na thamani kutokana na majanga ya ajali yanayotokea mara kwa mara Ziwani humo.
Mkandarasi Obuntu kutoka Uganda anatarajiwa kukamilisha ujenzi huo ndani ya mwaka mmoja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.