Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuleta mageuzi katika Sekta ya Ardhi nchini kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni jitihada za kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Katika hatua hiyo, Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 5 kununua jumla ya vifaa vya TEHAMA 1,429 ambavyo vitasambazwa katika Halmashauri 184 kote nchini.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika leo Januari 27, 2026 kwa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mwanza, Bw. Wilson Luge, amesema mkoa huo umepokea jumla ya vifaa 61.

Amesema kwa wastani kila Halmashauri imepatiwa kompyuta mbili, printa moja pamoja na UPS mbili, huku Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikipewa vifaa vya ziada ikiwemo kompyuta mbili zenye skrini, pamoja na simu za mezani kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano.

“Ni uwezeshaji mkubwa uliofanyika. Tunaamini kuongezeka kwa vifaa hivi kutapunguza changamoto ya uhaba wa vifaa uliokuwepo awali na kuboresha kwa kiasi kikubwa utendaji kazi,” amesema Bw. Luge.

Ameongeza kuwa Sekta ya Ardhi kwa sasa inatumia mfumo wa kielektroniki wa e-Ardhi, unaolenga kurahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi, na kwamba vifaa hivyo vitasaidia kuongeza kasi na ufanisi wa mfumo huo.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha miundombinu ya utoaji huduma katika sekta mbalimbali, ikiwemo Sekta ya Ardhi, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

“Vifaa hivi ni vingi na vimetumia gharama kubwa. Hata hivyo, havitakuwa na maana endapo huduma zitabaki kama zilivyokuwa awali. Matarajio yetu ni kuona maboresho ya dhahiri katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Bw. Balandya.

Katika hatua nyingine, Katibu Tawala ametoa onyo kwa watendaji wa sekta ya ardhi akisema hatarajii kuona vibali vya ujenzi vinatolewa katika maeneo yasiyoruhusiwa, wala kuwepo kwa umiliki wa ardhi kwa zaidi ya mtu mmoja, akibainisha kuwa mifumo ya kidijitali itaondoa changamoto hizo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.