SERIKALI YATOA BILIONI 56 KUIMARISHA USAFIRI WA VIVUKO NCHINI: WAZIRI ULEGA
Serikali imetoa jumla ya Tshs. bilioni 56 ili kuimarisha usafiri wa Vivuko 6, vitano vinakamilishwa Mwanza na kimoja Mafia mkoani Pwani lengo likiwa kuwaondolea adha ya usafiri wa maji wananchi wa maeneo ya visiwani.
Akizungumza mapema leo Januari 24, 2025 kwenye karakana ya Songoro wilayani Ilemela mkoani Mwanza vinapojengwa Vivuko 5 kwa gharama ya Tshs bilioni 21,Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega (MB) ambaye yupo ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miundombinu amebainisha tayari Serikali imetoa Tshs. bilioni 45 kuwalipa wakandarasi wanaodai kwenye miradi ili kuhakikisha kazi hizo zinakamilka kwa wakati.
"Nafurahi kuona maendeleo mazuri ya ujenzi wa Vivuko hivi, tayari siku ya jana nimeidhinisha fedha sasa ni imani yangu mkandarasi Songoro Marine kazi ya umaliziaji itakwenda vizuri", Waziri Ulega.
Amefafanua kuwa fedha hizo bilioni 56 ni pamoja na gharama ya Vivuko hivyo 6 ambayo ni shs bilioni 32.2 na fedha inayobaki ni gharama ya ukarabati wa Vivuko vya MV Kigamboni, MV Magogoni na MV Nyerere.
Kwa upande wake Meneja wa karakana hiyo Meja Songoro amesema vivuko hivyo vitano vipo katika hatua za mwishoni na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano mzuri",Songoro.
Aidha, Waziri Ulega ametoa maelekezo kwa Wakala wa ufundi na umeme,Tamesa wanaosimamia Vivuko hivyo kuhakikisha wanafanya usimamizi mzuri ili vyombo hivyo vya usafiri viwe na tija kwa wananchi.
Akiwa kwenye ukaguzi wa daraja la JP Magufuli lenye urefu wa km 3 na barabara unganishi ya km 1.66 lenye thamani ya zaidi ya shs bilioni 700, Waziri Ulega amesema tayari ameidhinisha malipo ya shs bilioni 16 kwa mkandarasi CCEC ili aweze kulikamilisha kama walivyokubaliana na Serikali Februari 28,2025.
"Mhe. Waziri daraja hili mbali ya kujengwa kitaalamu wa hali ya juu na kuwa daraja refu kwa nchi za Afrika Mashariki, pia litadumu kwa miaka 100 na sasa lipo katika hatua ya uwekeji lami",Mhandisi Dorothy Mtenga, Kaimu Mtendaji Mkuu, TANROADS.
Mhe. Abdallah Ulega hii ni ziara yake ya kwanza mkoani Mwanza akiwa Waziri wa Ujenzi akitokea Wizara ya Uvuvi na Mifugo aliyohamishiwa mwishoni mwa mwaka jana
.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.