Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) kuhakikisha inaendelea kuboresha bandari katika Ziwa Viktoria ili meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu iweze kutia nanga bila shida wakati itakapoanza safari zake.
Mwakibete ametoa maelekezo hayo leo Februari 12, 2023 jijini Mwanza baada ya kushuhudia meli hiyo kubwa ambayo itakuwa na mwendokasi zaidi kuliko meli zote zilizopo nchini ikiingizwa majini kwa mara ya kwanza katika bandari ya Mwanza Kusini iliyopo Wilaya ya Nyamagana itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo kwa wakati mmoja inayojengwa na mkandarasi kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 109.
.Amesema Serikali imekuwa ikiwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ya usafiri nchini lengo ni kuboresha huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria kwa wananchi wake hivyo itakapoanza kufanya safari zake kusiwepo na changamoto ya bandari kwenye maeneo itakayopita.
“Pia naielekeza Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL) kusimamia vyema menejimenti ya MSCL ili miradi yote inayotekelezwa na itakayotekelezwa na Serikali ileta thamani halisi ya fedha iliyowekezwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kusimamia mradi huu wa Ujenzi wa Meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu ukamilike ndani ya muda uliopangwa ili meli hii ianze kuwahudumia wananchi mapema iwezekanavyo,” amesisitiza Mhe. Mwakibete.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL, Mhandisi Eric Hamissi ujenzi wa Meli hiyo ambayo itafanya safari zake katika nchi zote ambazo ziko ukanda wa ziwa viktoria umekamilika kwa asilimia 82 na asilimia 12 zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne hadi mitano kuanzia sasa na kwamba hakuna changamoto ya fedha kwani hadi sasa Mkandarasi amekwishalipwa asilimia 88 ya gharama zake sawa na Sh bilioni 93.8 fedha iliyobaki tayari ipo kwenye akaunti wanasubiri amalize kazi ili waweze kummalizia malipo yake.
Amesema meli hiyo ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ina urefu wa mita 92.6, kimo ghorofa nne, upana mita 17 pia itakuwa na mwendo kasi tofauti na zingine zote ambazo zinafanya safari zake katika maziwa makuu hivyo itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo.
“Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu ikikamilika itakuwa ni kivutio kizuri sana tunataka watu wasafiri na kufanya utalii wakiwa safarini kwani ni ya tofauti kabisa itakuwa na uzito wa Tani 3500 leo tumeingiza majini tani 3000 hii ndiyo meli kubwa kuliko zote zinazoelea katika ukanda wa maziwa makuu.
“Hii Meli itakapokamilika itakuwa na madaraja sita ikiwemo daraja la hadhi ya juu kabisa(VVIP) daraja la watu mashuhuri(VIP),daraja la kwanza(first class) litabeba watu 60, daraja la pili (second class )abiria 200, daraja la biashara(business) abiria 100, daraja la uchumi lenyewe litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 834.
“Kutakuwa na lifti ambayo inauwezo wa kubeba watu 20 kwa wakati mmoja kwa ajili ya abiria ambao wanachangamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, migahawa ya kisasa, sehemu ya kucheza muziki, dispensary, ukumbi wenye uwezo wa kubeba watu 400 ambao wanaweza kufanyia sherehe humo kwa hivyo itakuwa ni kivutio kizuri sana ,,”ameeleza Mhandisi Hamissi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika hafla hiyo ya kusushwa majini kwa Meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu, Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa walisema kutekelezwa kwa mradi huo ambao umekuwa ni ndoto ya muda mrefu ya wananchi wao kunatarajiwa kuchagiza maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla kwani usafiri wa meli ni wa gharama nafuu zaidi pia unawezesha kusafirisha shehena kubwa kwa wakati mmoja.
“Wakazi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa tunakila sababu ya kumshukuru Rais wetu Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuendelea kuwekeza fedha nyingi sana katika mradi wa Meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu pamoja na miradi mingine ya maendeleo ya kimkakati iliyopo mikoa ya kanda ya ziwa,”amesema Mhe. Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.