Serikali imezindua rasmi msimu wa kilimo cha zao la pamba mkoani Mwanza huku ikitangaza kufanya operesheni ya kuwasaka vijana wanakaa vijiweni na kucheza michezo ya kubahatisha na kuwataka kufanya kazi.
Akizindua msimu huo kwa kupanda mbegu kwenye shamba darasa la kikundi cha Jikomboe katika Kijiji cha Gunge Kata ya mwaniko, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Mhe. Juma Sweda alisema kuanzia sasa hataki kuona wananchi wa kuzurula mitaani au kwenye baa.
Alisema kuanzia sasa anataka kuona wananchi ndani ya wilaya hiyo wakiwa mashambani na atakayekamatwa na kikosi cha operesheni ya kuwasaka wazembe mitaani na kupangiwa kazi ya kufanya ndani ya jamii kwa siku nzima bila malipo.
Mhe.Sweda alisema Serikali imejipanga kusimamia zao la pamba ili msimu wa 2019/2020 wakulima waweze kuvuna pamba yenye ubora wa kushindana soko la kimataifa ambapo aliwahakikishia uhakika wa soko.
“Kama mlivyoshuhudia nimezindua mimi kama Mkuu wa wilaya msimu wa upandaji mbegu za pamba, sasa kuanzia sasa kila mmoja aingie shambani na kuanza kupandikiza mbegu kwenye shamba lake, wito wangu kwa bwana shamba wa kila kata watoke ofisini na kwenda kwa wakulima ili kuwaelekeza namna ya kupanda kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba na itakapofika hatua ya kupalilia wafanye hivyo bila kusahau kupalilia mashamba yao.
“Naomba wananchi wasisahau mazao ya chakula, ni muhimu kuwa na zao la biashara na chakula hivyo yote kwa pamoja yanapaswa kwenda sambamba,naomba niwadokeze kuwa wakulima wengi wanashindwa kupata mazao mengi kwa sababu tunalima kienyeji, sasa mwaka huu nataka Misungwi tuwe mfano katika zao la pamba lenye ubora,”alisema Mhe.Sweda.
Kwa upande wa Afisa Kilimo na Umwagiliaji wa Misungwi, Majid Kabyemelwa alisema shamba darasa la kikundi cha Jikomboe lenye hekari mbili limekuwa mfano kwa wakulima wote ndani ya Wilaya ya Misungwi ambapo mwaka jana walivuna kilo 450 kwa hekari moja.
“Mwaka huu tumejipanga kulima hekari 15,940 ndani ya Wilaya ya Misungwi kwa msimu wa 2019/2020 ambapo nitahakikisha nawasimamia wataalaamu wangu kwenda mashambani kutoa elimu kwa wakulima ili tuvune pamba yenye ubora wa hali ya juu, naomba niwahakikishie hadi sasa hakuna mkulima anayedai fedha za pamba kwani zote zimeletwa,”alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Jikomboe, John Lugomeji alisema wamepata mafanikio makubwa kutokana na kilimo cha pamba ambapo baadhi ya wanachama wameweza kujenga nyumba za kisasa,kusomesha watoto, kuanzisha miradi ya biashara na kununua vitendea kazi vya kilimo.
“Pamoja na mafanikio hayo lakini kuna changamoto imejitokeza ya kuchelewesha malipo ya pamba, ndio maana ukichunguza kwa undani baadhi ya wakulima wamekataa kuanza maandalizi ya kuandaa mashamba yao na kudai kuwa uhakika wa soko haupo, hivyo tunaiomba Serikali kuleta wanunuzi wengi na sio mmoja,”alisema.
Aidha Bwana Shamba wa Kata ya Mwaniko, Sosteness Wabukoba alisema msimu wa 2018/2019, Serikali iliwalipa wakulima wa pamba Sh. milioni 60 katika vituo vya Nyasato, Gunge na Mwaniko.
Hata hivyo aliwaomba wakulima kuzingatia kanuni 10 za kilimo cha pamba msimu huu akisisitiza kuanzia sasa atakuwa anazunguka katika mashamba kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kupanda, kupalilia,kumwagilia dawa na mambo mengine kadri itakavyohitajika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.